Lipuli yaigomea Simba

Muktasari:

Miamba hiyo ya Iringa imefanikiwa kuvuna pointi mbili katika mechi zake mbili dhidi ya Simba msimu huu

Dar es Salaam. Lipuli imepunguza kasi ya Simba baada ya kulazimisha sare ya bao 1- 1 kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Matokeo hayo yanaifanya Lipuli kuweka rekodi ya kutofungwa na Simba msimu huu baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam kulazimishwa sare 1-1.

Lipuli ilicheza mbele ya mashabiki wake ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na mchezaji bora wa mwezi Adam Salamba katika dakika 31, baada ya kupokea mpira kutoka Mussa Nampaka na kisha kumtingisha beki wa Simba, Yusuph Mlipili kabla ya kuachia shuti kali upande wa kulia wa kipa Aishi Manula na kujaa wavuni.

Bao hilo la wenyeji Lipuli lilidumu hadi mapumziko katika kipindi cha pili mshambuliaji Laudit Mavugo aliyeingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya Juuko Murshid alisawazishia Simba akiunganisha kona ya Shomari Kapombe katika dakika ya 66.

Upangaji wa kikosi wa kocha wa Simba, Mfaransa Pierre Lecantre ni kama ulimponza hasa kipindi cha kwanza kwani hakukuwa na kiungo mchezeshaji hata mmoja zaidi ya kupanga wachezaji wengi ambao wanacheza nafasi ya ulinzi hivyo kuifanya Lipuli kutawala na kushambulia muda mwingi katika kipindi hicho. 

Lechantre aliwaanzisha kwa pamoja Nicholas Gyan kama beki wa kulia, Asante Kwasi (kushoto), mabeki wa kati Juuko Musrhid na Yusuph Mlipili, James Kotei, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe mabao wote ni wazuri katika kukaba na kujilinda kuliko kushambulia.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi 59, ikiwa mbele kwa pointi 12 kwa Yanga ambayo leo watashuka kwenye Uwanja wa Sokoine kuwavaa Mbeya City.

Kocha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alisema licha ya wachezaji wake kukabiliwa na uchovu, lakini watapambana kuhakikisha wanapanta pointi tatu na kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi.

Kocha wa Mbeya City, Ramadhan Nsanzurwimo alisema wako tayari kwa mchezo huo na wamepanga kulipa kisasi cha kuchapwa mabao 5-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam Novemba mwaka jana.