Lipuli yaapa kufuta rekodi ya Azam FC Uwanja wa Chamazi

Muktasari:

Lipuli imepanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara msimu huu, imeanza ligi vizuri kwani katika michezo mitatu iliyocheza mpaka sasa imeshinda mchezo mmoja na kutoa sare michezo miwili hivyo kujikusanyia pointi tano.

Dar es Salaam. Kocha msaidizi wa Lipuli, Amri Said amekiri kuwa  wana kazi ngumu kuikabiri Azam kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Lipuli imepanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara msimu huu, imeanza ligi vizuri kwani katika michezo mitatu iliyocheza mpaka sasa imeshinda mchezo mmoja na kutoa sare michezo miwili hivyo kujikusanyia pointi tano.
Said alisema anatambua jinsi Azam ilivyo timu bora kwenye ligi hiyo hivyo haitakuwa kazi rahisi kuifunga kirahisi lakini wamejiandaa kupata matokeo mazuri katika mchezo huo.
"Azam ni moja ya timu bora kwenye ligi hivyo haitakuwa mechi nyepesi na ukizingatia watakuwa kwenye uwanja wao hivyo lazima tujipange kikamilifu.
"Tumejiandaa vizuri kwa sababu tunataka kushinda mchezo huo. Ushindi unapatikana popote iwe nyumbani au ugenini muhimu ni juhudi tu za wachezaji. Tutapambana kuhakikisha tunaondoka na poiti tatu Jumapili," alisema Said.
Lipuli inakutana kesho na Azam ambayo mpaka sasa ndio timu pekee haijaruhusu nyavu zake kutikiswa tangu kuanza kwa Ligi Kuu  Agosti 26 .
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ni katika mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu huu na Azam kushinda mabao 4-0.