Ligi Daraja la Kwanza yazalisha mabao 218

Muktasari:

Huku jumla ya michezo ya raundi hizo tisa ikiwa ni 108, jumla ya mabao 218 inafanya wastani wa mabao kwa kila mechi iwe ni 2.02

JUMLA ya mabao 218 yamefungwa katika raundi tisa za Ligi Daraja la Kwanza ambayo mechi zake zimesimama hadi Disemba 16 kupisha kipindi cha usajili wa dirisha dogo kilichoanza rasmi Jumatano iliyopita. Huku jumla ya michezo ya raundi hizo tisa ikiwa ni 108, jumla ya mabao 218 inafanya wastani wa mabao kwa kila mechi iwe ni 2.02

huku kundi A likiwa kinara wa kuzalisha idadi kubwa ya mabao na kufuatiwa na kundi B.

Jumla ya mabao 82 ambayo ni sawa na 37.62% yamefungwa katika kundi A, mabao 70 ambayo ni sawa na 32.11% yamefungwa na timu zilizoko kwenye kundi B wakati mabao 66 ambayo ni asilimia 30.28 yamefungwa na timu nane zilizopo kwenye Kundi C.

Kwa mechi 36 zilizochezwa kwenye kila kundi, wastani wa mabao yanayofungwa katika kila mechi za kundi A ni 2.28, kwa Kundi B ni bao 1.94 wakati wastani wa mabao katika kila mechi za Kundi C ni bao 1.83.

Hadi ligi hiyo inakwenda mapumziko, timu inayoongoza kwa kupachika mabao mengi ni Maafande wa JKT Ruvu walioko Kundi A ambao wamefunga 18 wakifuatiwa na Alliance Schools inayonolewa na kipa wa zamani wa Tukuyu Star ya Mbeya, Mbwana Makata ina mabao 15. Timu tatu zinazoshika mkia kwenye ufungaji mabao ni Polisi Dar na JKT Oljoro zilizofunga mabao manne kila moja katika mechi tisa, zikifutiwa na JKT Mgambo, Rhino Rangers na Toto Africans ambazo hadi sasa kila moja imefunga mabao sita tu.