Lechantre apata dozi kuiua Yanga

Kocha wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre


VINARA wa Ligi Kuu Bara Simba wenye pointi 46, sawa na watani zao Yanga lakini wakiwa nyuma kwa mechi moja wameshaanza kupiga hezabu sahihi za kumaliza vizuri mechi 10, walizobaki nazo katika ligi kuu ili kufikia dhamira yao ya kuchukua ubingwa msimu huu.

Simba wamempa likizo ya wiki moja kocha wao mkuu Mfaransa Pierre Lechantre ambaye mara baada ya kumalizika mechi na Al Masry ambayo ilimalizika kwa sare ya bila kufunga alikwea pipa na kwenda likizo nchini kwao akiwa na familia yake.

Mmoja wa viongozi wa juu wa Simba alisema mechi na Al Masry ilikuwa ngumu na kocha wao Lechantre alitumia nguvu na akili nyingi ili kuhakikisha wanapata matokeo ya kusonga mbele kwenye mashindano haya lakini wakashindwa kufanya hivyo.

“Tuna mechi ngumu inayofaata ya ligi ambayo tunacheza na Yanga ili kuhakikisha tunashinda mechi hiyo tumeamua kumpa mapumziko ya wiki Lechantre ili kupata muda wa kupumzika na ikiludi awe na akili mpya ya kuiongoza timu kikamilifu kuelekea mechi hiyo,” alisema.

“Mechi na Yanga ni ngumu naimani kama Lechantre kwa muda ambao atakuwa amepumzika atakusanya mbinu nyingi na kupunguza makosa mengi ambayo tulifanya kwenye mechi na Al Masry ili katika maandalizi hayo tufanye kwa ukamilifu,” alisema kiongozi huyo.

Mratibu wa Yanga Abbas Ally alisema timu itaanza mazoezi Jumamosi katika Uwanja wa Boko Veterans chini ya makocha Masoud Djuma akisaidiana na kocha wa viungo Mohammed Habib na baada ya hapo kocha mkuu ndio atakuja kuungana na timu.

“Maandalizi ya mechi na Yanga yataanza Jumamosi na kama tutaenda kambi au kubaki hapa hapa Dar es Salaam litakuwa jukumu la kocha mkuu hapo atakapoludi atataka mazingira gani ya kujiandaa kuelekea mechi na Yanga,” alisema Abbas.

“Kila mechi kwetu ni ngumu na tunakutana na hasimu wetu na ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufanya vizuri msimu huu ni kushinda mechi hiyo kwani ni muhimu mno kwetu,” alisema.

Nahodha wa Simba John Bocco alisema wachezaji wapo mapumziko ya wiki moja lakini nafasi pekee iliyobaki msimu huu kufanya vizuri ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ili kushiriki mashindano ya Kimataifa msimu ujao.

“Kama wachezaji tunatambua kuwa tunajukumu kubwa mbele yetu ya kuchukua ubingwa wa ligi kwani ndio kiu kubwa ya kila mtu ndani ya Simba na tutapambana kwa hali na mali kuhakikisha tunalifanikisha hilo kwa kupata pointi katika kila mechi ambazo zimebaki,” alisema Bocco.