LECHANTRE, Hiyo mipango yake usipime

Muktasari:

Pembeni yangu wameketi Kocha Mkuu, Pierre Lechantre na Kocha wa viungo, Mohammed Al Habib, wakizungumza Kifaransa.

NI asubuhi moja yenye kaubaridi fulani hapa Port Said. Tunapata chai murua kwenye hoteli ya Nora and Style ilipofikia timu ya Simba. Ni chai nzito kweli kweli.

Pembeni yangu wameketi Kocha Mkuu, Pierre Lechantre na Kocha wa viungo, Mohammed Al Habib, wakizungumza Kifaransa.

Kama ulikuwa haufahamu Lechantre anazungumza Kiingereza na Kifaransa kwa ufasaha wakati Habib anazungumza Kiarabu na Kifaransa, hivyo Kifaransa ndicho kinawaweka pamoja muda mwingi.

Namalizia fundo mbili za chai yangu kisha nabeba glasi ya juisi na kusogea mezani kwao. Nataka kuzungumza machache na Lechantre, ambaye muda mwingi anaonekana kuwa bize tangu tulipotua hapa toka Tanzania.

Naanza kwa kumuuliza hali ya mashindano ya kimataifa kwa mwaka huu anaionaje, kuna kitu gani kimemkosha mpaka sasa.

“Hatukuwa na safari nzuri sana kule Djibouti, vitu vingi havikwenda sawa, lakini hapa Misri naona tumeimarika zaidi. Kama unavyofahamu Simba haikuwa imeshiriki mashindano haya kwa muda mrefu hivyo, inahitaji kuendelea kujifunza,” ndivyo alivyoanza kusema.

“Hatukuwa na matokeo mazuri sana dhidi ya Al Masry nyumbani hivyo tulijiweka kwenye mazingira magumu ya kucheza ugenini ili kutafuta ushindi.”

Namtazama kwa makini zaidi kocha huyu ambaye hutabasamu kwa nadra, kisha namuuliza namna alivyoikuta timu na ilivyo sasa baada ya kuiongoza kwenye mechi 10 za mashindano yote bila kupoteza mchezo hata mmoja.

“Tatizo kubwa wakati tumefika hapa wachezaji wengi hawakuwa na utimamu mkubwa wa mwili,” anasema Lechantre, ambaye amewahi kuipa Cameroon taji la Afrika mwaka 2000.

“Mfano Laudit Mavugo hakuwa fiti kabisa. Imebidi nimpe Habib (kocha wa viungo) kazi ya kumsaidia na sasa naona ameanza kuimarika japo sio kwa kiwango ninachokitaka.

“Nadhani timu haikuwa na maandalizi mazuri ya utimamu wa mwili mwanzoni mwa msimu.

“Niliuliza marafiki zangu waliopo Afrika Kusini kama waliona timu ikifanya maandalizi ya kutosha mwanzoni mwa msimu, wakasema hapana.

“Wachezaji wengi hawana uwezo wa kucheza mechi nyingi mfululizo, hatuna uwezo wa kucheza kila baada ya siku tatu, tunachoka. Mfano Shomari Kapombe alicheza vizuri kwenye mechi nne, lakini ya tano akasema amechoka na kweli asingeweza kuwa kwenye kiwango bora. Tulimpumzisha na mechi iliyofuata alicheza vizuri.

“Endapo tutaendelea kuwa hapa itabidi tufanye maandalizi makubwa zaidi mwanzoni mwa msimu ujao, hayo ndiyo yanatoa taswira ya msimu mzima.”

KAPOMBE KIUNGO

Hapo hapo nakumbuka kuhusu beki Kapombe kuhamishwa nafasi na kupangwa kiungo, eneo ambalo hakuwahi kulicheza kwa miaka ya karibuni.

“Ana nguvu na kasi nzuri. Pia ana uwezo mkubwa wa kukaba na ndiyo sababu nimemsogeza kwenye eneo hilo. Pia, timu ikizidiwa anarudi kusaidia kukaba upande wa beki ya kulia,” anasema kocha huyo.

“Tatizo kubwa hapa tuna viungo wengi washambuliaji kuliko wakabaji. Wengi wakishika mpira wanakuwa wazuri, lakini wakipoteza hawana habari. Mfano Said Ndemla ni kiungo mzuri lakini akiwa na mpira, akishapoteza siyo kazi yake kuutafuta.

“Wengi wapo taratibu katika kukaba, sasa kwenye mechi za kimataifa huwezi kufanya vizuri kama kila mchezaji hakabi, hilo ni soka la zamani yaani mchezaji mmoja anataka wengine wakabe kisha wampe mpira acheze. Leonel Messi ni mchezaji bora zaidi duniani kwa sasa, lakini Barcelona ikipoteza mpira utamuona anakwenda kukaba.

“Ninachoshagaa ni kwamba, kocha aliyetangulia hapa aliwezaje kuwa na viungo washambuliaji wengi, ama ndiyo aina ya wachezaji aliowahitaji?,” anazungumza Lechantre huku usoni akionyesha kuwa siriazi.

KWASI NA GYAN

Mabadiliko mengine ambayo yamefanyika kwenye kikosi cha Lechantre ni kumtumia mshambuliaji Nicholas Gyan katika nafasi ya beki wa kulia na Asante Kwasi beki wa kushoto. Namuuliza Lechantre aliona nini ambacho makocha wengine hawakukiona kwa nyota hawa?

“Gyan ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa. Anakaba, anakokota mpira na anatumia akili kubwa sana na ndiyo sababu nimempa uhuru wa kujaribu kwenda mbele kila wakati.

“Unajua napenda soka la kushambulia kupitia pembeni hivyo, nahitaji wachezaji wenye nguvu pembeni na ndiyo maana upande wa kushoto anacheza Asante Kwasi, ambaye naye yuko vizuri,” anaeleza Lechantre.

OKWI, BOCCO

Mazungumzo yetu yanaendelea kwa kasi kidogo, Lechantre anaonekana kuwa na mengi na anawazungumzia mastaa; Emmanuel Okwi na John Bocco.

“Ni wachezaji hatari hasa kwenye ushambuliaji. Naweza kusema tuna wachezaji wa daraja la juu kwa Tanzania katika eneo la ushambuliaji,” anasema.

“Ubaya ni kwamba kuna tofauti kubwa baina yao na mastraika wengine. Mfano kwenye mechi dhidi ya Stand United tuliwakosa wote wawili, ilikuwa majanga tu.

“Unapowakosa Bocco na Okwi ukitazama nyuma nani acheze unaumwa na tumbo. Mavugo hayuko kwenye utimamu wa mwili wa kutosha japokuwa ameanza kuimarika na atakuwa vizuri muda si mrefu.

“Ukitazama Mosses Kitandu ni chipukizi bado, si mchezaji wa kumbebesha mzigo mzito. Juma (Liuzio) hakuwa tayari kucheza hivyo, ilikuwa ni pigo kubwa kwetu, ilibidi tupange tu waliokuwepo,” anaeleza kwa hisia kali kidogo huku akihoji: “Kuna wachezaji hapa Simba sijui hata wamefikaje.”

MBIO ZA UBINGWA

Mbio za ubingwa Ligi Kuu Bara zilianza kama mzaha vile. Simba ilikuwa mbele ya Yanga kwa pointi saba. Zikapungua na kuwa tano, zikapungua tena na kuwa tatu na sasa timu hizo zimelingana alama 46 kileleni.

Uhodari wa Bocco, Kichuya na Okwi kwenye kufunga ndiyo umeifanya Simba iendelee kukaa kileleni kwa wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kuhusu mbio hizo, Lechantre anasema: “Tunahitaji kuongeza kiwango, wachezaji wawe na uwezo wa kucheza mechi moja kila baada ya siku tatu ili tusiwe matatizoni lala salama hii.”