Kwa ngumi zile! Mwakinyo kavuta pesa hii

Muktasari:

Si unajua Mwakinyo kwa sasa ndio habari ya mjini, baada ya kumchapa kwa TKO raundi ya pili tu ya pambano la raundi 10, Muingereza Sam Eggington na kushtua dunia kutokana na rekodi matata za Eggington, ambaye alikuwa nafasi ya nane kwenye ubora duniani kwa mabondia wa uzani wa super welter.

HAPA ndio utafahamu kwanini wanamichezo wa Kibongo wanakufa masikini! Yaani kama ulikuwa unapigia hesabu mkwanja wa bondia Hassan Mwakinyo ili kumpiga mzinga basi acha kabisa kwani, jamaa wala hajavuta pesa ya maana kabisa licha ya kumshushia mpinzani wake ngumi nzito mwanzo mwisho.

Si unajua Mwakinyo kwa sasa ndio habari ya mjini, baada ya kumchapa kwa TKO raundi ya pili tu ya pambano la raundi 10, Muingereza Sam Eggington na kushtua dunia kutokana na rekodi matata za Eggington, ambaye alikuwa nafasi ya nane kwenye ubora duniani kwa mabondia wa uzani wa super welter.

Sasa unaambiwa mkwanja alioingiza Mwakinyo ni Dola za Marekani 3,000 tu (Sh 6.6 milioni).

“Watu wanaweza kuziona ndogo, lakini wakati anakwenda kucheza Uingereza hakuwa staa hadi aliposhinda ndiyo amepata umaarufu, hivyo pambano linalofuata atalipwa fedha nyingi zaidi,” alisema Juma Ndambile, ambaye kampuni yake ya Don Chief Promotion ndiyo ilitafuta pambano hilo.

Alisema kuwa kwenye ngumi za kulipwa, malipo ya bondia sio baada ya pambano ni kabla ya pambano na hata ikitokea umepigwa fedha yako iko pale pale.

Mwakinyo anatua nchini kesho Ijumaa na tayari Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema mapokezi makubwa yanamsubiri.

“Alichokifanya Mwakinyo ni heshima na niseme tu mbali na mapokezi tukayompa, pia tutakaa naye ili tuone namna ya kumsaidia na kumuandaa kimkakati ili aweze kufika mbali,” alisema Dk. Mwakyembe.

REKODI ZA MWAKINYO

Achana na mapokezi hayo, lakini taarifa ni kuwa bondia huyo hajaibukia tu Uingereza, jamaa amewahi kukosa mkanda wa ubingwa wa dunia wa WBC katika pambano lililofanyika Desemba 2, 2017 jijini Moscow. Katika pambano hilo, Mwakinyo alizichapa na Lendrush Akopian kuwania ubingwa wa WBC kwa vijana katika uzani wa super feather pambano la raundi 10, ambapo alimaliza raundi zote na mpinzani wake kupewa ushindi kwa pointi.

“Pambano hili ndilo lilinipa funzo kuwa, ukizipiga ugenini na kumaliza kwa pointi huwezi kushinda, kifupi ili ndilo lilinipa mzuka wa kushinda kwa KO nje ya nchi,” alisema Mwakinyo.

Pia, ana mkanda wa ubingwa wa WBA Pan African ambapo alimchapa bondia wa Botswana, Anthony Jarmann kwa TKO raundi ya saba ya pambano la raundi 10 lililopigwa jijini Gaborone.

Tangu ameingia kwenye ndondi mwaka 2015, Mwakinyo amepigwa mara mbili tu na Akopian kwa pointi kule Russia na Shaban Kaoneka hapa Bongo kwa KO raundi ya sita mwaka 2015, lakini akalipa kisasi kwa Kaoneka mwaka mmoja baadaye kwa kumchapa kwa KO raundi ya kwanza na hadi sasa ana rekodi ya kushinda mara 12 (8 kwa KO) na kupigwa mara mbili (1 KO).

Mama afichua siri ya Mwanaye

Fatma Hassan ni mama mzazi wa Mwakinyo, ambaye amefichua siri ya mafanikio ya mwanaye ni kuwa mchezo huo upo ndani ya familia. Amesema kuwa baba yao ndiye aliyebeba siri hiyo kwani, aliwaletea vifaa kutoka nchini Kuwait kwa kuwa, alikuwa akipenda sana hivyo, watoto wameurithi.

Akizungumza na Mwanaspoti nyumbani kwake eneo la Makorora mjini Tanga, mama huyo alisema kuwa: “Baba yao ambaye ni marehemu kwa sasa aliporejea kutoka Kuwait alikoishi kwa miaka 10, alikuja na vifaa vya mchezo wa ngumi na kuwakabidhi Hassan pamoja na kaka yake, Hamis,” alisema Fatma.

Alisema amepokea kwa furaha kubwa taarifa za mwanaye kushinda nchini Uingereza, kwani wakati akiondoka alibaki na kazi ya kumwombea kwa Mungu.

“Siku ambayo aliniaga kuwa anakwenda kupigana Uingereza aliniomba niwe namsomea dua ili Mungu amjaalie kupata ushindi, na nilifanya hivyo nashukuru Mungu amesikia sala zetu,” aliongeza.

Kwa upande wake Hamis, ambaye ni kaka na kocha wake Mwakinyo alisema juhudi za mchezo wowote duniani ni kuwa na nidhamu ya mazoezi, ndiyo siri kubwa ya ushindi wa mdogo wake.

“Mwakinyo ana nidhamu ya hali ya juu anapokuwa ulingoni, uwezo wake hauna shaka kwa sababu hata mazoezi anajituma sana,” alisema.

Vijana wa maskani ya Domozege iliyopo Makorora, Tanga wengi wamemwelezea Mwakinyo kwamba, ni bondia anayejituma kwenye mazoezi na kuwa ushindi huo ni sehemu ya kuwa na nidhamu.

Pia, wamesema kuwa Mwakinyo ni tofauti na mabondia wengine kwani, amekuwa akijiepusha na vitendo vya kihuni na kuendekeza anasa na kwamba, hana kawaida ya kujichanganya na magenge ya kihuni.