Kwa hawa Waethiopia, Yanga ni wao tu

Muktasari:

Kwa miaka mfululizo, Yanga imekuwa ikipangwa dhidi ya timu hizo na kuangukia pua.

NANI anatamani kupangwa na timu za Waarabu kwenye mashindano ya Afrika? Zinatisha bana, asikwambie mtu.

Kwa miaka mfululizo, Yanga imekuwa ikipangwa dhidi ya timu hizo na kuangukia pua.

Itakumbukwa, ilipangwa na Al Ahly (Misri), Etoile Du Sahel (Morocco) na MC Alger kwa siku za karibuni na ikaangukia pua. Inauma kweli kweli.

Hata hivyo, Mwenyezi Mungu siyo mchoyo wa fadhila. Mwaka huu Mungu ameiepusha Yanga mbali na Waarabu hao wa Kaskazini. Baada ya kuwashindwa Township Rollers ya Botswana, Yanga sasa imepewa Wahabeshi wa hapo Ethiopia tu.

Ni timu ya Welayta Dicha iliyofuzu hatua hiyo kwa kukiondosha kigogo cha soka Afrika, Zamalek ya Misri ambayo Yanga inaiogoa kama mtoto mdogo anavyoogopa moto. Mechi hizo za mchujo kombe la Shirikisho Afrika sasa zitapigwa kuanzia Aprili 6 na Yanga itaanzia hapo Taifa na baadaye kwenda Addis Ababa kwa marudiano.

Baada ya droo hiyo iliyofanyika pale Cairo, Misri usiku wa juzi Jumatano, watu wa Yanga wametabasamu.

Kinachowapa matumaini mashabiki wa Yanga na Watanzania kwa ujumla ni historia ya miaka 20 iliyopita ambapo Yanga ilifanikiwa kuitoa timu ya Coffee kutoka Ethiopia kwa ushindi wa jumla wa mabao 6-3 na kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998.

Pamoja na yote, wadau wengi wa soka nchini hawaifahamu sana hii timu ya Ethiopia lakini kidogo wameingia upepo wakisikia imeiondosha Zamalek. Ifahamu timu hiyo kwa undani.

Ina miaka 9 tu

Tofauti na Yanga ambayo ni moja ya timu kongwe barani Afrika ikiwa na miaka 83 tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 1935, Dicha ni timu changa, sio tu Afrika bali hata nchini kwao Ethiopia.

Timu hiyo ilianzishwa rasmi mwaka 2009 na haina zaidi ya misimu saba katika Ligi Kuu ya Ethiopia hivyo kwa suala la uzoefu, Yanga ina uzoefu mkubwa wa soka la Afrika mbele ya Dicha kwa zaidi ya mara 20.

Kwa hapa Tanzania, timu hiyo ni changa kuliko hata Azam FC ambayo ilianzishwa mwaka 2007 na 2008 ikaanza kushiriki Ligi Kuu. Jina la utani la timu hiyo linaitwa ‘Nyuki wa Sona’

Jezi kama Yanga

Wahabeshi hao wanatumia rangi tatu za jezi ambao kuu ni kijani na njano pamoja na rangi nyeusi ambazo huwa za bukta pale wanapovaa jezi za rangi ya njano juu.

Rangi hizo za jezi ndizo ambazo zimezoeleka kutumiwa na Yanga katika mashindano na nyakati mbalimbali kutegemea na rangi za jezi kwa timu pinzani wanayokabiliana nayo.

Wanachama 73,000

Pamoja na uchanga wake, timu hiyo imemudu kushawishi kundi kubwa la mashabiki kuipenda na kuifanya iwe miongoni mwa klabu zenye idadi kubwa ya mashabiki nchini Ethiopia nyuma ya timu za Saint George, Coffee, Dedebit, Awassa City na Adama City.

Kwa mujibu wa mtandao wa klabu hiyo, jumla ya wanachama waliosajiliwa na walio hai wa timu hiyo ni 73,000.

Idadi kubwa ya wanachama wa Dicha wanapatikana katika Mji Mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa ambako ndiko makao makuu ya klabu hiyo yapo.

Watolewa jasho Zanzibar

Wengi wanaihofia Dicha baada ya kusikia wameitoa Zamalek ya Misri ambayo ni moja ya timu kongwe na zenye historia kubwa barani Afrika lakini walichokisahau ni kwamba Wahabeshi hao nusura watupwe nje na wawakilishi wa Zanzibar kwenye mashindano hayo, timu ya Zimamoto.

Ingawa walifanikiwa kupenya na kuingia hatua iliyofuata, Dicha walilala na viatu mbele ya Zimamoto kwani katika mechi ya kwanza walitoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Amaan kabla ya kushinda nyumbani kwa bao 1-0. Na hata hilo bao lenyewe moja walilolipata nyumbani lilitokana na penati.

hawatumii uwanja

Uwanja wa nyumbani wa Wolayta Dicha unaitwa Sodo ambao huwa wanautumia kwa ajili ya mechi za ndani lakini kwenye mashindano ya kimataifa wanalazimika kutumia Uwanja wa timu ya Awassa City kutokana na ule wa kwao kutokukidhi viwango vya mechi za kimataifa vilivyowekwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Uwanja huo wanaoutumia kwa mechi za kimataifa ambao Yanga watakwenda kuuchezea, upo kwenye mji wa Awassa uliopo Kusini mwa Ethiopia, umbali wa zaidi ya Kilomita 273 kutoka Mji Mkuu wa Addis Ababa.

Wageni watatu tu

Tofauti na Yanga ambayo ina wachezaji sita wa kigeni, Dicha ina wachezaji watatu tu ambao wanatokea nje ya Ethiopia ambao ni kipa, Emmanuel Favour Obhyo kutoka Nigeria, Kiliouto Asselmo Massama wa Chad na Arafat Djako kutoka Togo.

Tathmini inaonyesha kuwa kama kuna mchezaji ambaye Yanga wanapaswa kumchunga zaidi kwenye kikosi cha Wahabeshi hao basi ni mshambuliaji Djako ambaye ni raia wa Togo.

Djako ndiye kwa kiasi kikubwa amechangia kuifikisha Dicha kwenye hatua hiyo akifunga mabao mawili nyumbani na ugenini dhidi ya Zimamoto.

Usifike matuta

Yanga inapaswa kumaliza biashara yao mapema kabisa katika dakika za kawaida za mchezo vinginevyo huenda ikajikuta kwenye wakati mgumu iwapo mshindi baina yake na Dicha atalazimika kupatikana kwa mikwaju ya penati.

Rekodi zinaonyesha kwamba walimng’oa Zamalek kwa mikwaju ya penati lakini pia mikwaju ya penati ndio iliwabeba hadi wakafanikiwa kutwaa Kombe la Ethiopia kwa ushindi wa matuta walipoifunga Defence Force kwa penalti 4-3.

Pia kwenye nusu fainali ya kombe hilo walishinda kwa mikwaju ya penati dhidi ya Ethio-Electric.

Yanga ikitaka itaabike, basi wafike kwenye matuta, japokuwa ujio wa mastaa wake, wanaweza kufanya kitu.