Kwa Simba hii nunueni suti kabisa

Thursday August 10 2017Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog 

By Mwandishi wetu

MABOSI wa Simba wameanza kutabasamu baada ya kubaini kuwa namna walivyousuka ukuta wa timu yao, ili wapinzani wapate bao ni wazi kwamba wanahitaji kupita juu.

Simba imesajili mabeki sita wa maana ambao wameungana na mabeki watatu waliokuwepo klabuni hapo hivyo kuufanya ukuta wa timu hiyo kuwa wa chuma hasa baada ya kucheza dakika 270 na kuruhusu bao moja pekee tena dhidi ya timu za maana.

Licha ya kwamba safu ya ushambuliaji ya Simba bado haijapata makali ya kutosha, gumzo kubwa limekuwa katika safu ya ulinzi ambayo katika michezo miwili ya kirafiki iliyopita wamecheza dhidi ya mabingwa wa Afrika Kusini, Bidvest Wits na mabingwa wa Rwanda, Rayon Sports bila kuruhusu bao.

Katika kuhakikisha ukuta huo unasimama imara, Kocha Joseph Omog aliamua kumpa unahodha Mzimbabwe, Method Mwanjali ambaye anasimama katika beki ya kati sambamba na Salim Mbonde ama Juuko Murshid.

Kiwango hicho cha safu ya ulinzi kimeipa Simba kiburi kwamba inaweza kupata matokeo dhidi ya timu yoyote hasa wapinzani wao Yanga ambao watafungua nao pazi la Ligi Kuu katika mchezo wa Ngao ya Jamii Agosti 23.

Uwepo wa washambuliaji wengi wenye uwezo wa juu umempagawisha kocha Omog ambaye kwenye mchezo wa juzi dhidi ya Rayon Sports aliamua kumpanga mshambuliaji, Emmanuel Okwi katikati ili kutoa fursa kwa Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim kucheza Pembeni.

Okwi alionyesha kiwango cha juu akicheza nyuma ya straika John Bocco jambo ambalo linamfanya Mrundi, Laudit Mavugo sambamba na Mghana, Nicholas Gyan kuanzia nje.

Hata hivyo viwango cha Mavugo na Gyan vinaifanya Simba nayo kuwa na safu imara ya ushambuliaji sawa na ile ya watani zao Yanga ambao kwa misimu miwili mfululizo wamekuwa vinara wa mabao.

PASI ZA NIYONZIMA

Uwepo wa viungo wengi wenye uwezo wa kukaba ndani ya Simba kama Mzamiru Yassin, James Kotei, Said Ndemla na Jonas Mkude huenda ukamfanya kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima kucheza kwa kiwango cha juu kuliko wakati akiwa Yanga.

Katika mechi dhidi ya Rayon, Niyonzima alionyesha uwezo mkubwa wa kupiga pasi za kupenyeza ambazo washambuliaji Gyan na Bocco walishindwa kuzifanya ziwe mabao. Niyonzima alionekana kucheza kwa uhuru zaidi ya alivyokuwa Yanga na viungo wakabaji walikuwa na viwango vya kawaida.

BOCCO

“Bado tupo katika kutengeneza timu, kuna kombinesheni zimeanza kuonekana lakini bado hatujafikia kiwango bora. Naamini tutafanya vizuri sana,” alisema Bocco.

“Nilifanya vizuri nikiwa na Azam lakini nina deni hapa. Tuna kazi kubwa ya kufanya kama timu ili msimu ukianza tuwe vizuri zaidi,” aliongeza

OKWI

Kwa upande wa Okwi alisema; “Nilichogundua sasa kikosi chetu kina wachezaji bora na sasa hatutaki heshima hiyo ibaki katika majina yetu tunataka mafanikio kwa kuipa mataji Simba.

“Nimefurahi kumuona mtu mwenye uwezo kama Haruna (Niyonzima) nimeungana naye tena hapa Simba niliwahi kucheza naye pale Yanga ninamfahamu vyema uwezo wake, anajua kutengeneza nafasi na hata kufunga ukiongeza na Kichuya nafikiri tunapaswa kupata mafanikio makubwa.

“Hiki ni kikosi kipana ambacho kinakuwa na mchanganyiko wa vipaji vya hali ya juu Wanasimba wanataka mafanikio ambayo waliyakosa kwa muda mrefu kwa kikosi hiki hakuna sababu ambayo itatufanya tushindwe kufanya hivyo.”