Kuwafunga Simba ni kazi aisee!

Muktasari:

Kocha wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre amekuwa akiwachezesha wachezaji saba ambao, kiuhalisia ni mabeki na ikitokea wamepungua sita lazima wawepo katika timu.

UKIKITAZAMA vizuri kikosi cha Simba, utagundua kuwa kati ya wachezaji 11 wanaunda kikosi cha kwanza, saba ni mabeki na wanne waliobaki mmoja kipa na watatu tu ndiyo washambulia staili ambayo kwa timu pinzani kuwafunga lazima ufanye kazi ya ziada.

Kocha wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre amekuwa akiwachezesha wachezaji saba ambao, kiuhalisia ni mabeki na ikitokea wamepungua sita lazima wawepo katika timu.

Simba ambayo inamtumia mlinda mlango wao, Aishi Manula katika mechi zote za ligi, kutokana na mfumo wao wa 3-5-2 au 4-4-2 imekuwa ikiwachezesha mabeki wa kati asili watatu hadi wanne badala ya wawili kama zinavyofanya timu nyingine.

Piga ua katika kikosi cha Lechantre huwezi kuwakosa, Juuko Murshid, Yusuph Mlipili, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na Asante Kwasi mbali na hao Mfaransa huyo humjumuisha Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na James Kotei katika kikosi kimoja,

Amefanya hivyo katika mechi tofauti ikiwemo ile ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons kwa kuwachezesha sita na watano waliobaki alikuwa mlinda mlango Aishi Manula, kiungo Jonas Mkude na John Bocco, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya.

Akitumia mfumo wa 3-5-2 akichanganya na 4-4-2 Juuko, Mlipili na Nyoni walicheza nyuma na pembeni kulikuwa na Tshabalala pamoja na Kapombe, winga ya kushoto alicheza Kwasi, Mkude kati na kulia Kichuya wakati washambuliaji wa kati alicheza Bocco na Okwi na baadaye alimtoa Kwasi akamuingiza Kotei. Upo uwezekano mkubwa mechi ya kesho Jumamosi dhidi ya Lipuli wakacheza hivyo kwa sababu Lechantre amesisitiza hataki kupoteza nafasi hata moja.

Wakati mwingine Lechantre amekuwa akimchezesha mshambuliaji Nicholas Gyan kwenye beki lengo likiwa ni kutoa krosi nzuri za mwisho kutokea pembeni na washambuliaji wafunge na hata anapokuwa huyo, Kapombe huwa anampandisha kucheza kiungo.

Lechantre amesema: “Watu hawaoni kama tunacheza mpira wa kushambulia kutokana na mfumo wetu ambao ni 3-5-2, lakini mpira tunaocheza ni wa kushambulia pamoja na kuzuia.”

Kocha wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohamed ‘Bares’ amesema: “Kwa aina ya mfumo huu huo ambao Simba wanacheza iko wazi kocha anataka matokeo.