Kunguru hafugiki; Lechantre asepa

Muktasari:

  • Hilo limetimia baada ya Mfaransa huyo aliyetambulishwa kwa mbwembwe nyingi kuchukua nafasi ya Mcameroon Joseph Omog kuamua kuikacha timu ikiwa katikati ya mashindano.

Dar es Salaam. Januari 19, 2018, mashabiki wa Simba walilipuka kwa shangwe baada ya ujio wa kocha Pierre Lechantre, lakini Mfaransa huyo hajawahi kukaa katika klabu moja zaidi ya mwaka.
Hilo limetimia baada ya Mfaransa huyo aliyetambulishwa kwa mbwembwe nyingi kuchukua nafasi ya Mcameroon Joseph Omog kuamua kuikacha timu ikiwa katikati ya mashindano.
Lechantre ameondoka Simba ikidai ni kutokana na kushinda kuelewana na baadhi ya viongozi juu ya mahitaji, lakini pia suala la kiwango cha timu hiyo katika siku za karibuni pamoja na kufanikiwa kutwaa ubingwa.
Hata hivyo kwa anayemjua kocha Lechantre hawezi kushangaa kwa sababu rekodi zake zinaonyesha hajawahi kufundisha zaidi ya mwaka tangu alipoondoka Cameroon 2001 baada ya kuipa ubingwa wa Mataifa ya Afrika mwaka 2000.
Kwa mujibu wa mtandao wa http://www-herzog.transfermarkt.kr unajihusisha na kutoa takwimu za masuala mbalimbali ya michezo umeonyesha kocha Lechantre anawastani wakufundisha timu si chini ya mwaka kabla ya kuondoka.
Mfaransa huyo aliwashangaza watu pale alipoamua kuvunja mkataba wake wa kuifundisha Senegal wiki mbili baada ya kukubali kuchukua jukumu hilo mwaka 2012.
Mfaransa huyo aliimbia Senegal press agency (APS)“Nilipata mkataba wiki iliyopita, lakini hiyo siyo kigezo pekee cha mimi kuendelea na jukumu langu la kuiongoza timu ya Senegal kama wameshindwa kunitimizia matakwa yangu.”
Viongozi wa Senegal walishindwa kumlipa mshahara wake wa miezi sita aliyotaka kulipwa kwanza kabla ya kuanza kazi.
Mfaransa huyo alianza kufundisha Afrika na timu ya taifa ya Cameroon kuanzia (Jan 1, 1999) hadi (Jun 30, 2001) sawa na siku (911).
Baada ya hapo akatimkika Qatar akaifundisha timu ya taifa ya nchi hiyo kuanzia (Agosti 1, 2001)     hadi (Desemba 31, 2001)sawa na siku 152.
Akajiunga kuifundisha klabu ya  Al Ahli ya Qatar alidumua nayo kwa siku 123 tu kuanzia(Julai 1, 2003) hadi (Novemba 1, 2003) kabla ya kutimkia timu nyingine ya Al Sailiya ya Qatar aliyokaa kwa siku 242 kuanzia(Nov 1, 2003) hadi (Jun 30, 2004).
Lechantre alirejea Afrika baada ya kupata mkataba wa kuifundisha Mali kwa muda mfupi kwa lengo la kuwapa tiketi ya Kombe la Dunia 2006, alifundisha hapo kwa siku 240 kuanzia (Machi 5, 2005) hadi (Okt 31, 2005).
Baada ya kushindwa kuipeleka Mali katika Kombe la Dunia 2006, Lechantre alitimkia katika klabu ya Al Rayyan ya Qatar akifundisha kwa siku 276, kuanzia(Okt 1, 2006) hadi (Jul 4, 2007).
Kuanzia Julai 4, 2007 hadi Desemba 31, 2007 alibukia Morocco na kujiunga na klabu ya MAS Fes aliyodumu nayo kwa siku 180 tu.
Club Africain ya Tunisia ilimchukua Mfaransa huyo  kuanzia Juni 12, 2009 hadi Aprili 8, 2010. Ndiyo klabu aliyokaa kwa muda mrefu zaidi alidumu kwa siku 300, baada ya kuiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya pili na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mafanikio aliyoyapata Club Africain yalivutia miamba mingine ya Tunisia, CS Sfaxien aliyokaa kwa siku 166 kuanzia Juni 22, 2010 hadi Desemba 5, 2010 kabla ya kutupiwa virago.
Baada ya kuchemsha Tunisia akatimkia Qatar na kujiunga na klabu ya Al Gharafa aliyokaa kwa siku 196, kuanzia Machi 19, 2012 hadi Oktoba 1, 2012.
Kocha Lechantre aliweka rekodi ya kufundisha siku 39, katika klabu ya Al Arabi ya Qatar kuanzia Machi 19, 2012 hadi Aprili 27,  2012. Baada ya kuondoka Qatar aliibukia Libya na kujiunga na klabu ya Al-Ittihad    aliyokaa kwa siku 187,kuanzia Machi 30, 2015 hadi Oktoba 3, 2015.
Kocha huyo mwenye bahati ya kufundisha mataifa ya Afrika, alipata ulaji Januari 13, 2016 wa kuifundisha Congo Brazzaville, lakini mkataba huo ulivunjwa ikiwa bado una miezi 17 mbele.
Novemba 15,2016, Congo ilitangaza kuvunja mkataba wake na kocha Lechantre baada ya kufungwa na Uganda 1-0 na kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018.