Kumekucha Man City, Liverpool, Chelsea, Arsenal kukiwasha

Muktasari:

  • Jana Manchester United ilikuwa na shughuli pevu huko Old Trafford ilipoikaribisha Leicester City na hiyo ilikuwa mechi ya kufungua pazia la Ligi Kuu England, ambapo kila kocha anajaribu kusaka njia za kuubeba ubingwa ambao msimu uliopita ulinyakuliwa na Manchester City ya Pep Guardiola.

LONDON, ENGLAND. HUKO England kumenoga, ni amshaamsha tu. Ile mikikimikiki ya Ligi Kuu England imerudi rasmi, usiku wa jana Ijumaa kulikuwa na mechi moja, lakini uhondo kamili unaanza leo Jumamosi na kuendelea kesho Jumapili.

Jana Manchester United ilikuwa na shughuli pevu huko Old Trafford ilipoikaribisha Leicester City na hiyo ilikuwa mechi ya kufungua pazia la Ligi Kuu England, ambapo kila kocha anajaribu kusaka njia za kuubeba ubingwa ambao msimu uliopita ulinyakuliwa na Manchester City ya Pep Guardiola.

Utamu wa ligi hiyo kwa timu za Top Six kwa msimu huu ni kwamba kutakuwa na makocha wawili wageni, Unai Emery huko Arsenal na Maurizio Sarri huko Chelsea.

Makocha hao wanakuja kuwapa changamoto wenyeji wao, Guardiola wa Man City, Jose Mourinho wa Man United, Jurgen Klopp wa Liverpool na Mauricio Pochettino wa Tottenham Hotspur.

Mchakamchaka wa msimu huu utashuhudia pia mastaa wa kigeni kibao wakitua kwenye Ligi Kuu England kuongeza uhondo utakaofanya utamu wa michuano hiyo pengine kuzidi misimu uliopita.

Mechi ya kwanza itakayofanyika mchana wa leo Jumamosi, Newcastle United inayonolewa na Rafa Benitez itakuwa nyumbani kuikaribisha Spurs, mechi inayotazamwa itakuwa ngumu kwelikweli kabla ya Bournemouth kumaliza ubishi na Cardiff City, Fulham ikiwa na mastaa wapya kibao wakishuka uwanjani kucheza na Crystal Palace, Watford ikicheza na Brighton na Wolves itakuwa na kasheshe mbele ya Everton. Kocha Sarri ataanzia shughuli ya Ligi Kuu England ugenini wakati atakapoifuata Huddersfield.

Lakini yote hiyo ni tisa, kumi bana ni vipute vya hiyo kesho Jumapili. Huko Emirates kutakuwa na kasheshe zito, wakati Emery na chama lake la Arsenal watakapowakaribisha mabingwa watetezi Man City.

 Mechi hiyo inatarajia kuwa na ufundi mkubwa, huku Arsenal ikiingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa Tatu Bila katika mechi ya mwisho ya ligi ilipocheza uwanjani Emirates dhidi ya vijana hao wa Guardiola.

Lakini mechi hiyo ya baadaye, itatanguliwa na mechi mbili matata, wakati Liverpool itakapokuwa Anfield kuikaribisha West Ham United, ambayo imefanya usajili mkubwa sana kwenye dirisha lililofungwa juzi Alhamisi.

Mechi nyingine itakayopigwa kesho ni ile ya Southampton itakapocheza na Burnely. Macho ya mashabiki baada ya kuona ile shughuli ya Man United usiku wa jana, sasa watasubiri kuona kipi kitafanywa na Chelsea, Tottenham, Man City na Arsenal kwenye mechi zao. Mambo ni moto!