Kumekucha! Piga chini Ngoma bakisha Chirwa

Muktasari:

  • Kocha huyo kijana amekiangalia kikosi cha Yanga hasa safu yao ya ushambuliaji kisha akashtukia kwanini timu hiyo imekuwa ikifanya vyema, huku ikiwa inatumia mamilioni ya fedha kuwalipa nyota wa kigeni wasiofanya kazi Jangwani.

YANGA imerejea nchini kutoka Botswana, lakini kama kuna kitu ambacho mabosi wake wanapaswa kukizingatia ni ushauri waliopewa na Kocha Bora wa Tanzania msimu uliopita, Mecky Maxime.

Kocha huyo kijana amekiangalia kikosi cha Yanga hasa safu yao ya ushambuliaji kisha akashtukia kwanini timu hiyo imekuwa ikifanya vyema, huku ikiwa inatumia mamilioni ya fedha kuwalipa nyota wa kigeni wasiofanya kazi Jangwani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Maxime alisema Yanga inaonekana kuwa na matokeo mazuri yanayowashangaza wengi lakini tatizo ni ubora wa Chirwa ambaye hakuna beki anayeweza kumdhibiti hapa nchini.

Maxime alisema Chirwa sio mtu mzuri kwa mabeki hasa wa hapa nchini ambao haoni kama kuna mtu anaweza kumdhibiti kutokana na kujaliwa vitu vingi vinavyompa ubora wa kuwa tishio.

Akasema kama inataka kuwa wakali zaidi ni lazima imteme Donald Ngoma aliye mfanyakazi hewa Jangwani na kumpa mkataba wa maana Chirwa ili aendelee kuwabeba.

Beki huyo na nahodha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars alisema Chirwa hazuiliki kwa beki mmoja au wawili lakini pia kasi yake na akili yake katika kujua kutulia na kufunga ndiyo silaha kubwa ambayo inawapa ubora Yanga. “Unajua watu wanaiangalia Yanga kwa jicho tofauti nikweli Yanga inaonekana kuwa na matatizo mengi lakini hayo ni mambo ya nje ya uwanja ubora wa Yanga upo uwanjani na tatizo ni yule Chirwa,” alisema Maxime.

“Chirwa amekuwa mhimili mkubwa wa Yanga katika kuipa ubora yule sio mshambuliaji wa kumlinganisha ni kama Okwi sema Chirwa anachomzidi Okwi ni akili na nguvu.”