Kumbe ule mchongo wa wanariadha feki ulikuwa hivi!

UNAKUMBUKA lile sakata la wanariadha feki walionyimwa visa kwenda Norway na Poland? Sasa, sikia kumbe mchongo wake ulianza hivi!

Awali Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Riadha (RT), Rehema Kilo ndiye alitajwa kutoa kibali cha RT kwa mtu aliyedai ni wakala wa wanariadha.

“Nilipewa maelekezo na Mama Zavalla (Ombeni ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa RT),” alisema Killo na kuendelea.

“Aliniambia kuna wakala atanipigia simu anataka wanariadha, hivyo nimsaidie kwa kuwa yeye hayupo amesafiri kwenda Ujerumani.”

Anasema baada ya siku mbili kweli wakala huyo alimpigia simu akiomba amsaidie wanariadha watakaokwenda kwenye mbio Poland na Norway.

“Nilimwambia mimi wanariadha sina, ila nikamuunganisha na makocha wawili wa Arusha ambao sijui alizungumza nao nini hadi nilipokuja kusikia amenyimwa visa, lakini kibali cha RT mimi sikumpa na sijui alikipata wapi,” alisema Killo.

Mama Zavalla alipoulizwa alisema kibali hicho kiliandikwa na Katibu Muhtasi wa RT, Rachel Swai kwa maelekezo ya Katibu wa Kamati ya Ufundi ya RT.

“Mimi kwanza sikuwepo nchini wakati mchakato huo unafanyika, nilikuwa Ujerumani hivyo ishu hiyo anaweza kuizungumzia vizuri Gidabuday (Wilhelm ambaye ni Katibu Mkuu wa RT),” alisema Zavalla.

Hivi karibu wakala huyo alinyimwa visa ya kuwapeleka watu 12 nchini Norway na Poland alikodai wanakwenda kwenye mbio ingawa 10 kati yao hawakuwa wanariadha.

“Nilipigiwa simu na maofisa ubalozi ambao walitia shaka, nilipotajiwa majina ya wanariadha, niliwatambua wawili pekee, hivyo nikawaambia wazuie visa zao,” alisema Gidabuday alipoulizwa juu ya suala hilo.

Alisema watendaji wa RT waliohusika kumpa mtu aliyedai ni wakala kibali cha RT watajadiliwa kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji baadaye Juni.