Kumbe mchawi Djuma

Masoud Djuma

Muktasari:

  • Lechantre hakuwepo kwenye benchi juzi Alhamisi wakati Simba ikiiondosha Kakamega Homeboys kwenye nusu fainali ya SportPesa Super Cup, kabla ya usiku kusafiri na kurejea Dar es Salaam.

DAR ES SALAAM. KOCHA Mfaransa, Pierre Lechantre, ameondoka mjini Nakuru hapa Kenya na kurejea Dar es Salaam kumalizana na mabosi wa Simba ambao wamekubaliana kwa kauli moja kuachana naye.

Lechantre hakuwepo kwenye benchi juzi Alhamisi wakati Simba ikiiondosha Kakamega Homeboys kwenye nusu fainali ya SportPesa Super Cup, kabla ya usiku kusafiri na kurejea Dar es Salaam.

Pamoja na mwenyewe kutokuwa tayari kuzungumzia hatma yake klabuni hapo, lakini aliweka wazi kuwa si kocha wa Simba kwa sasa kwa kuwa mkataba wake umemalizika na hajapewa mkataba mpya.

“Mimi si kocha wa Simba kwa sasa, mkataba wangu umemalizika na sijafahamu kama nitaendelea kuwepo hapa ama la,” alisema Lechantre kabla ya kurejea Dar es Salaam.

Pamoja na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ kushindwa kuwa na ufafanuzi wa moja kwa moja, lakini taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata ni kuwa kocha huyo amekwenda Dar es Salaam kuchukua stahiki zake kisha anarejea zake kwao Ufaransa.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tully, alisema kocha huyo amekwenda Dar es Salaam lakini kuhusu hatma yake itafahamika huko.

“Siwezi kusema kama tumeachana naye, amekwenda Dar es Salaam ambako atakutana na viongozi wa juu wa ili kufahamu kitakachoendelea,” alisema Tully.

Wakati viongozi wa Simba wakiwa na kigugumizi kuweka wazi kilichomkuta kocha huyo, habari za uhakika ni kwamba wameshindwana naye na anaondoka huku mchakato wa kusaka kocha mpya ukianza.

Sababu kubwa inayomwondoa kocha huyo ni Simba kucheza soka la kujilinda kwa muda mwingi, jambo ambalo limewakera mashabiki pamoja na viongozi.

Pia, inaelezwa kuwa Lechantre amekuwa na uhasama na msaidizi wake, Masoud Djuma na amekuwa hachukui ushauri wowote kwake.

Pamoja na hilo amekuwa akimtaka Djuma asizungumze lolote na wachezaji bila kuomba ruhusa kwake, huku akigoma kufanyia kazi ushauri wowote kutoka kwa viongozi wa Simba pamoja na kocha huyo msaidizi.

“Ilifikia hatua kwamba Djuma akimwambia kocha kitu inakuwa ugomvi, anamwambia mimi ni kocha mkuu, nafanya ninachoona ni sahihi,” alisema mmoja wa viongozi wa Simba.

“Mfano Masoud alimwambia kwenye mechi dhidi ya timu hizi za kawaida Simba inatakiwa kushambulia, lakini akagoma na kupanga kikosi cha kujilinda. Simba si timu ya hivyo.”

Kutokana na mgogoro huo mkubwa uliokuwepo dhidi ya msaidizi wake, Lechantre alimkataza pia Djuma kusimama kwenye benchi wakati mchezo wowote ukiendelea kwa madai kuwa, anaingilia majukumu yake.

“Masoud alikuwa akizungumza na wachezaji ili kuwapa hamasa, lakini Lechantre alikuwa hapendi hivyo. Wachezaji waliokuwa karibu na Masoud aliwaita wachezaji wa kocha huyo, ni mambo ya kiswahili,” aliongeza kigogo huyo.

Pamoja na hayo, sababu nyingine kubwa ambayo imemwondoa kocha huyo Simba ni gharama kubwa za kumlipa na kumpa malazi nchini, ambapo Simba hutumia zaidi ya Sh40 milioni kila mwezi kwa ajili yake tu.

Kiwango hicho cha fedha kimeonekana kuwa kikubwa ukilinganisha na kipato cha timu hiyo ambacho kwa mwezi si zaidi ya Sh160 milioni.

Wasikilize hawa

Staa wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella, ameonyesha kushangazwa na taarifa za Lechantre kuachana na mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu Bara, akisema zinaweza kurudisha nyuma maendeleo ya timu uwanjani.

“Ukiona timua timua ya makocha imezidi ujue wapo viongozi ambao, wanafanya makusudi kusajili walimu ambao hawatakaa nao kwa muda mrefu ili wakitimuliwa watafute wengine na kuendelea kuishi mjini.

“Simba kwa sasa ina uwekezaji mzuri, ila isipokuwa makini itafeli katika uongozi kwani itaendeleza kasumba yao ya kuchukua watu ambao hawana viwango vya timu, hili waliangalie kwa kina,” alisema.

Hakuishia hapo, Mogella alikwenda mbali zaidi kuzungumzia usajili wa wachezaji akishauri kuwa ni lazima kuwepo na vipengele vya kupima malengo na kama visipofikiwa basi mikataba ivunjwe.

“Mtazame Okwi (Emmanuel) hana maajabu sana, lakini anacheza kwa malengo baada ya kuwasoma wachezaji wa Kitanzania kuona hawajui wanataka nini uwanjani.”

Naye mchambuzi makini wa soka la Tanzania, Ally Mayay ‘Tembele’ aliwashauri Simba kuwa kama wameachana na Lechantre basi wasitishe usajili hadi watakapopata mrithi wake.

“Mipango yao sijui ni nini, lakini kama wamemuondoa basi wasubiri kocha mpya, ambaye watampa timu ndiye asajili kulingana na maono yake, lakini wakisajili tu anaweza kuja mwalimu na mahitaji tofauti kabisa na walivyofanya wao, hapo ndio shida hutokeza,” alisema.