Kumbe Wazee Simba hawataniwi

Friday August 11 2017

 

By JAMES MAGAI

WIKI moja iliyopita Wazee wa Simba kupitia Bodi ya Wadhamini walitishia kuzuia Mkutano Mkuu wa klabu hiyo uliopangwa kufanyika Jumapili hii, lakini watu wakadhani labda ni mkwara tu, kumbe bwana hawakuwa wakitania.

Wadhamini hao wametinga mahakamani na kufungua kesi ya kuupinga mkutano huo ambao lengo kubwa lilikuwa ni kupitisha mabadiliko ya katiba ambayo yangeruhusu mfumo mpya wa uwekezaji klabuni hapo.

Bodi hiyo ya Wadhamini inayoongozwa na nyota na kiongozi wa zamani wa Simba, Hamis Kilomoni, imefungua kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakiomba mahakama hiyo izuie kufanyika kwa mkutano huo.

Wakili wa bodi hiyo ya wadhamini, Juma Nassoro amelieleza Mwanaspoti kuwa, kesi hiyo ilitarajiwa kusikilizwa leo Ijumaa mchana na Hakimu Thomas Simba.

Kabla ya kufikia uamuzi huo wa kufungua kesi, bodi hiyo ya wadhamini iliuonya uongozi wa klabu hiyo kuachana na mipango ya maandalizi ya mkutano huo na kwamba kama wakiendelea basi itakwenda mahakamani kuuzuia. Uamuzi huo wa Bodi ya Wadhamini ni kinyume na kanuni za Shirikisho la Soka duniani (Fifa) inayokataza masuala ya soka kwenda mahakamani hivyo kuna uwezekano wa Simba ikapoteza nafasi ya kushiriki Ligi Kuu pamoja na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kama bodi hiyo itashikilia msimamo wake.