Kuelekea Kiev: Kumbe Real Madrid hawana ubavu kwa Liverpool

Muktasari:

Real Madrid ndiyo mabingwa watetezi, wanacheza mechi hiyo wakiwa na ndoto ya kulibeba kombe hilo kwa mara ya tatu mfululizo, wanajivunia  kuwa na mshambuliaji, Cristiano Rinaldo na kocha wao, Zinedine Zidane.

Kiev, Ukraine. Saa 3:45 usiku wa leo Jumamosi, macho na masikio yataelekezwa katika dimba la NSC  Olimpiyskiy au maarufu kama Olympic Stadium, lenye uwezo wa kuingiza watazamaji wapatao 70,000, ingawa Uefa wanasema, watazamaji 63,000 tu ndio watakaoruhusiwa kuingia uwanjani.
Unaambiwa dunia itasimama kwa takribani dakika 90, pale Jiji la Kiev, litakaposhuhudia rekodi mpya na historia ikiandikwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Naam! Mabingwa watetezi, Real Madrid watakuwa na kibarua cha kutetea ubingwa wao dhidi ya Liverpool.
Los Blancos, wataweza kuwazuia watoto wa Malkia? Hilo jibu hata mimi sina ila rekodi mbona iko wazi mwanangu? Huna habari? Acha nikodokeze kidogo. Fainali ya leo, itakuwa ni mechi ya sita inayokutanisha miamba hii miwili katika historia ya michuano hii.
Unajua ilikuaje? Tulia nikupe data mwanawani. Katika mara zote sita walipokutana Real Madrid, walipigika kinoma unaambiwa. Katika mechi sita, Liverpool imeibuka kidedea mara tatu.
Madrid wao wameshinda mara mbili tu. Yaani waswahili wanakuambia, Los Blancos walichezea 3-2. Mbona tunabishana sasa, lakini? Najua huamini. Ili nikuoneshe kuwa Mwanaspoti huwa hatuzungumzi bila data, hizi hapa ni mechi tano za awali.
Kombe la Uropa (European Cup Final)- Liverpool 1-0 Real Madrid. Mechi hii ilipigwa Mei 27, 1981. Ikiwa ni fainali yao ya tatu katika kipindi cha miaka mitatu, baada ya kushinda fainali za 1977 na 78, Liverpool walikuwa na ndoto kubwa ya kufuata nyayo za Nottingham Forest huku wakiwa na kiu ya kuipa ujiko England kwa kuwa taifa la kwanza kutwaa taji hilo mara tano mfululizo.
Vijana wa Malkia, wakaliamsha dude balaa unaambiwa, ambapo katika dakika ya 82, Alan Kennedy aliuzamisha wavuni, Real Madrid wakatulia tuli. Ushindi huo ukamuingiza Bob Paisley, kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kuweka rekodi ya kuwa Kocha wa kwanza kubeba taji hilo mara tatu mtawalia.
Kumbuka wakati huu, kombe hili lilikuwa bado linajulikina kama Kombe la Ulaya (European Cup). Maana kuna wanangu fulani wa mabanda umiza walishaanza kuvimba kwa jazba!
Ligi ya mabingwa Ulaya, hatua ya 16 bora- Real Madrid 0-1 Liverpool (Februari 25, 2009)
Kama kuna usiku ambao Mhispania Rafael Benitez, atazidi  kuukumbuka katika maisha yake, basi ni ule usiku alipowavuruga Real Madrid pale Santiago Bernabeu. Licha ya kumkosa Nahodha wake Steven Gerrard, Liverpool waliupiga mwingi asikwambie mtu na kuhakikisha Los Blancos wanaloa 1-0 nyumbani.  
Usiku ule, Muizraeli mwenye roho ngumu Yossi Benayoun alitakata balaa. Mwanaume yule, katili yule, aliuzamisha bila hofu. Akiunganisha krosi ya Fabio Aurelio, katika dakika za lala salama, Benayoun alihakikisha Bernabeu inatulia na kuimba jina lake yeye.
Ligi ya mabingwa, hatua ya 16 bora- Liverpool 4-0 Real Madrid (March 10, 2009)
Kama uliamini shughuli aliyokabidhiwa Benitez na vijana wake, ya kuwaangamiza Real Madrid iliishia pale Bernabeu, basi inawezekana kabisa ulilogwa wewe. Moto uliowashwa kule Anfield hadi shetani aliogopa. Dunia ilisimama!
Watoto wa Malkia walitinga hatua ya Robo fainali kwa staili ya aina yake. 'Captain Fantastic' Steven Gerrard, alihakikisha anawabeba wanae mgongoni. Alitupia mara mbili wavuni, huku Fernando Torres na Andrea Dossena wakitupia mengine mawili. Los Blancos wakala mvua 4-0!
Ligi ya mabingwa, hatua ya makundi- Liverpool 0-3 Real Madrid (Oktoba 22, 2014).
Nani anakubali kuonea kizembe? Real Madrid walisema basi inatosha. Miaka mitano baada ya mechi tatu za uonevu, Los Blancos, walisafiri hadi Anfield, kukutana na wababe wao hao, katika mechi ya hatua ya makundi.
Liverpool walikuwa ndio kwanza wamerudi baada ya kukaa nje ya michuano hii kwa zaidi ya miaka minne.  Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, tayari Liverpool walishapigwa 'tatu mzuka'.  Wafungaji wakiwa ni Cristiano Ronaldo na Karim Benzema aliyetupia wavuni mara mbili.
Ligi ya mabingwa, hatua ya makundi- Real Madrid 1-0 Liverpool (Novemba 4, 2014).Baada ya kula 3-0 nyumbani, Brendan Rogers alisafiri na kikosi chake hadi Santiago Bernabeu, huku akiamua kutowatumia Gerrard na Raheem Sterling. Alikuwa anawahifadhi kwa ajili ya mechi ya EPL dhidi ya Chelsea. Karim Benzema akawaua kwa goli pekee na la ushindi. Wakaaga mashindano kwa aibu.
Wawili hawa wanakutana tena usiku wa leo. Kila timu iko imara. Liverpool wanaenda Kiev wakijivunia uwepo wa Klopp kwenye benchi la ufundi huku uwanjani wakiendelea kufurahia kiwango kizuri cha Mohammed Salah na wenzake, Sadio Mane na Roberto Firmino.
Kwa upande wao, Real Madrid wanajivunia kuwa mabingwa watetezi, ndoto ya kulibeba mara tatu mfululizo, lakini pia wana mtu anayeitwa Cristiano Rinaldo bila kumsahau Kocha wao, Zinedine Zidane. Yote tisa, kumi tukutane Kiev baadae!