Kumbe Mo Salah si chaguo la Klopp

Muktasari:

Mchezaji ambaye Klopp alitaka aletewe kwenye kikosi chake ni staa wa Bayer Leverkusen, Julian Brandt

LIVERPOOL, ENGLAND. UNAAMBIWA hivi, Jurgen Klopp hajawahi kuwa na mpango wa kumsajili Mohamed Salah na supastaa huyo yupo Anfield kwa sasa bila ya mapendekezo ya kocha huyo.
Ni hivi, mabosi wa Liverpool wamedai kwamba ni wao ndio waliamua kumsajili Mo Salah, lakini Klopp yeye kulikuwa na orodha ya wachezaji wengine kabisa aliotaka wanaswe kwenye kikosi chake huko Anfield.
Mchezaji ambaye Klopp alitaka aletewe kwenye kikosi chake ni staa wa Bayer Leverkusen, Julian Brandt, lakini bodi inayoshughulika na mambo ya usajili, iliamua kwenda kumsajili Mo Salah bila ya matakwa ya kocha.
Lakini, mwisho wa yote ni kwamba Mo Salah amekwenda kufanya huduma bora kabisa kwenye kikosi cha Liverpool na kumpa raha kocha Klopp.
Kwenye msimu wake wa kwanza tu huko Anfield, Mo Salah alifunga mabao 44, huku akibeba Kiatu cha Dhahabu cha England na mabao yake 32 na sasa yupo kwenye orodha ya wakali watatu wanaowania tuzo ya Fifa ya mchezaji bora wa mwaka.