Kumbe Lema bonge la staa!

Muktasari:

  • Kucheza soka kwenye klabu hiyo kumemfanya Lema kuzungumzwa kila kona, jambo ambalo mwenyewe limempa mzuka kwelikweli.

KUMBE ishu yenyewe ndio iko hivi. Yule winga wa kimataifa wa Tanzania, Michael Lema (18) anayekipiga klabu ya SK Sturm Graz inayoshiriki Ligi Kuu Austria, ni bonge la supastaa unaambiwa.

Kucheza soka kwenye klabu hiyo kumemfanya Lema kuzungumzwa kila kona, jambo ambalo mwenyewe limempa mzuka kwelikweli.

Lema, aliyezaliwa na kukulia Itigi mkoani Singida, alitua nchini humo kimasomo na alipewa nafasi klabuni hapo kutokana na kuonyesha kipaji kikubwa.

“Soka limenifanya kuwa staa mkubwa na kufahamiana na watu, wenzetu wamelipa kipaumbele soka la vijana ambao, nilicheza timu ya vijana wa timu B ambayo kuna ligi wanashiriki za madaraja ya chini.

“Upande wa Ligi hizo nilifanya vizuri na kuwa mchezaji bora, kuanzia hapo ndiyo mashabiki wakaanza kunijua na kunizungumzia,” alisema Lema.

Hata hivyo, Lema ni miongoni mwa wachezaji wachache wa kikosi B ambao, wamepata nafasi ya kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza kwa lengo la kujengewa uzoefu.