Kumbe Kapombe kahusika dili la Nyoni

YANGA bado hawaamini imekuwaje hata wakamkosa beki kiraka, Erasto Nyoni aliyekwenda kutua Simba waliotumia saa mbili tu kumbadili mawazo, lakini huku nyuma imebainika kumbe Shomari Kapombe ndiye chanzo cha kila kitu.

Kapombe aliyecheza na Nyoni ndani ya Azam FC ndiye aliyemchomoa kiraka huyo katika uelekeo wa Yanga ili akatue Msimbazi.

Ipo hivi. Taarifa kutoka kwa mmoja wa mabosi wa Simba ni kwamba mpaka juzi Jumatano asubuhi Yanga walikuwa na uhakika wa kumnasa Nyoni, lakini saa mbili baada ya Wekundu kumalizana na kipa Said Mohamed ‘Nduda’, akili za haraka zikawasukuma kumsajili mchezaji huyo baada ya kutishwa na majeraha ya Kapombe.

Kapombe amesajiliwa Simba hivi karibuni lakini mabosi wa Simba wametonywa kuwa beki huyo si wa kumtegemea sana kutokana na rekodi za majeraha ya kila mara, ndipo kura zikamwangukia Nyoni aliyekuwa huru.