Kocha riadha atoa neno la mwisho

Arusha: Timu ya riadha inayokwenda kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola inatarajia kuondoka Jumapili Arusha kwenda Dar es Salaam kwaajili ya kuungana na wenzao wa michezo mingine.

 Kocha Mkuu wa timu hiyo Zakaria Barie alisema baada ya kukabidhiwa bendera watajumuika na wenzao kwaajili ya safari kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere wiki ijayo.

 “Tumepata kila kitu kwa muda tuliokuwa kambini tangu Februari 8, wakati kambi ikiwa na wanariadha 15 na baadaye tukabaki tisa baada ya wengine kuondoka na kila kitu kilienda safi na matumaini ya kufanya vyema yapo” alisema Barie.

 Aliongeza hadi sasa hakuna mwanariadha wenye tatizo kiafya kwa kuwa wote wapo na moyo wa kwenda kushindana katika mashindano hayo yanayotarajia kuanza April nne hadi 15 katika jiji la Gold Coast nchini Australia.

Pamoja na hayo alieleza kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo Lwiza John hakuwepo kwa siku chache kutokana na kupata tatizo la kifamilia lililomsababisha kuondoka kambini.

 Nahodha wa timu hiyo mwanariadha Said Makula aliwaondoa wasiwasi Watanzania kwa kueleza kuwa watakwenda kufanya vyema kwenye mashindano hayo licha ya changamoto zilizojitokeza hapo nyuma.

“Kila mtu anawaza lake kuhusu mashindano haya, lakini siri kubwa ya mwanariadha ni kujiaandaa mwenyewe kwa asilimia 75 huku zilizobaki ndizo zinakuwa za kocha” alisema Makula.

 Wanariadha Sita wanatarajia kwenda kupeperusha bendera ya Tanzania ambao ni Stephano Huche, Said Makula na Sara Ramadhan kwa upande wa mbio ndefu, wengine ni Failuna Abdi 10,000 M, Ally Gulam 100 M na 200M pamoja na Anthony Mwanga wa mbio za miruko.