Kocha Transit Camp anajiamini kinoma noma FDL

Muktasari:

Timu sita za daraja la kwanza zitapata daraja mwisho wa msimu huu

Mwanza. Kocha Mkuu wa Transit Camp, Nevelin Kanza amesema timu za Biashara, Dodoma na Alliance FC zisijipe kiburi kupanda Ligi Kuu kwa kuwa nafasi tatu za juu, kwani hata wao wanayo nafasi ya kucheza ligi hiyo msimu ujao.

Camp yenye maskani yake mjini Shinyanga, ilimaliza mechi zake tisa ikiwa nafasi ya sita kwa pointi 10 kwenye msimamo wa ligi Daraja la kwanza kundi lao C.

Kanza alisema hadi sasa hakuna anayeweza kutanua kwapa kuwa anauhakika wa kupanda Ligi Kuu, kwani ni pointi ndogo ambazo timu zinazidiana.

“Hawa waliopo nafasi tatu za juu wasitambe, hadi sasa hakuna anayeweza kumtambia mwenzake, bado Trans Camp tunayo nafasi ya kupanda hadi nafasi ya pili kama tutashinda mechi zetu”alisema.

Kocha huyo aliongeza kuwa kwa kipindi hiki cha dirisha dogo, wataongeza wachezaji wanne, katika nafasi ya kipa, beki wa kushoto na wa kati pamoja na kiungo mshambuliaji.

Alisema kuwa nafasi waliyopo siyo nzuri, hivyo wanahitaji watakaoongezwa waje kubadili matokeo na kwamba usajili wao ni askari kama zilivyo taratibu na kanuni za timu za majeshi. 

“Wachezaji tutakaoongeza tutawatoa kwenye kituo chetu cha michezo cha Tuwalipo kilichopo Dar es Salaam, ambao wana uwezo, hatutapunguza mchezaji yeyote”alisema kocha huyo.