Kocha Pluijm amkumbuka Chilunda

Muktasari:

  • Chilunda aliukosa mchezo huo ambao Azam ilishinda mabao 2-0 yaliyopatikana muda wa nyongeza kwa vile klabu anayoenda kuichezea ya Tenerife ya Hispania kumzuia ikihofia asiumie.

KOCHA wa Azam, Hans Pluijm, amekiri kukosekana kwa straika wake chipukizi, Shaaban Idd Chilunda katika mechi yao dhidi ya Gor Mahia kulichangia kupata ushindi hafifu, japo wanafurahia wametinga fainali ya Kombe la Kagame.

Chilunda aliukosa mchezo huo ambao Azam ilishinda mabao 2-0 yaliyopatikana muda wa nyongeza kwa vile klabu anayoenda kuichezea ya Tenerife ya Hispania kumzuia ikihofia asiumie.

“Kukosekana kwa ghafla kwa Chilunda imetuumiza kwani alikuwa mtu sahihi katika kipindi hiki, hata hivyo washambuliaji wengine waliobakia nao ni wazuri naamini tutafanya kitu kizuri zaidi kwenye mchezo wetu ujao,”alisema Pluijm.

Akizungumzia mchezo wao wa leo wa fainali dhidi ya Simba, alisema hana presha na mchezo kwa sababu timu zote zinazocheza ni za Tanzania na yupo tayari kwa matokeo yoyote katika mchezo huo.

Simba na Azam zinacheza fainali na zina uhakika wa kulibakisha kombe nyumbani kwani mshindi wa mchezo wa leo ataweka heshimba nyumbani.