Kocha Odhiambo ataja kilichoiponza Bandari

Tuesday June 26 2018

 

By ABDULRAHMAN SHERIFF

Mombasa. KAMA alivyoonya mapema Kocha Mkuu wa Bandari FC, Ken Odhiambo kuwa mechi za maondoano zina utata wake, hivyo ndivyo ilivyotokea timu yake ilipobanduliwa nje ya Mashindano ya SportPesa Shield kwa kuchapwa mabao 3-1 na Tusker FC.

Odhiambo aliwaonya wachezaji wake siku mbili kabla mechi kuchezwa kuwa wasicheze kwa mbwembwe kwani wakitingwa, watakuwa wametolewa mashindanoni. Baada ya dakika 90 za mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Mbaraki Sports Club, mkufunzi huyo alikubali kushindwa.

Lakini alikubali kuwa ameshindwa kutokana na siku hiyo kuwa mbaya kwao na wala si kwa sababu wachezaji wake walicheza kwa madoido ama kuwadharau wapinzani wao hao wa Tusker.

“Vijana wangu walifuata onyo langu la awali la kutocheza kwa mbwembwe na kuwadharau wapinzani wetu, walicheza kwa bidii lakini siku haikuwa yetu bahati ilituelemea na ndio tukapoteza mchezo huo,” alisema Odhiambo.

Alisema matukio mawili katika mchezo huo ndiyo yaliyowadhuru na kusababisha kufungwa kwao. “Tulijifunga bao la kusawazisha la Tusker kutokana na mpira uliomponyoka kipa wetu na sababu nyingine ni kupoteza mkwaju wa penalti ambao ungelitufanya tuongoze mabao 2-1,” alisema.

Hata hivyo, Odhiambo alisema matokeo ya mchezo huo sasa ni sawa na maji tayari yaliyomwagika, hayazoleki tena. “Sasa tuko kujitayarisha kwa mechi zetu za Ligi Kuu ya SportPesa mbazo tutajitahidi tushinde nyingi ama zote zilizobakia,” aliongeza mkufunzi huyo.

Na kocha mwenzake wa Tusker FC, Robert Matano alisema vijana wake walianza kwa upole mno lakini kila dakika zilipokatika, walichangamka na kustahili kupata ushindi.

 “Tulistahili ushindi kwani tulicheza vizuri zaidi ya wapinzani wetu ambao ni wagumu hasa nyumbani kwao,” alisema Matano.

Timu hiyo ya Tusker imefanikiwa kuwa mojawapo ya timu bora zitakazopigania ushindi kwenye mechi zitakazohusisha timu 16. Tusker ilianza kwa kuitandika Taita Taveta All Stars FC mabao 7-0 wiki mbili zilizopita na kufuzu kupambana na Bandari.