Kocha Njombe aumia kwa kufungwa nyumbani

Muktasari:

Njombe Mji imepanda daraja msimu huu na bado haipo katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi

Dar es Salaam. Kocha wa Njombe Mji, Mlage Kabange amekiri kipigo alichokipa kutoka kwa Azam FC, imeharibu ramani katika kuhakikisha anamaliza nafasi nzuri ya msimamo wa ligi.

Njombe ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Azam mwishoni mwa wiki jambo linalomfanya kocha Kabange kusema wangeshinda na Azam, ingewasaidia kuwa kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi.

"Tumeshinda mchezo mmoja tu dhidi ya Majimaji ya Songea, tumetoka sare baadhi na kufungwa, hii kwetu inatuweka njia panda, tulitarajia mchezo wetu na Azam, angalau ungetubeba.

"Inaumiza kufungwa nyumbani ambako mashabiki wana uwezo wa kuja kwa wingi, mwisho wa siku wanarejea majumbani wakiwa na maumivu makali,"alisema.

Lakini alijipa moyo na kuendelea kujipanga kwa mechi tano zilzosalia kabla ya kuingia mzunguko wa pili kwamba huenda zikawaweka kwenye nafasi nzuri.

"Naendelea kuwajenga wachezaji waangalie mbele zaidi, hatuna budi kuendeleza mapambano kwani safari bado ni ndefu, inayohitaji uvumilivu wa hali ya juu,"alisema.