Kocha Mwadui aleta nyota wa Nigeria, Ghana

Muktasari:

  • Kocha huyo aliyekuwa katika mapumziko mafupi kwao nchini Rwanda alitua juzi Alhamisi akiwa na nyota hao tayari kwa kuanza kazi klabuni hapo.

Mwanza. Mtawakoma Mwadui! Ndivyo unaweza kusema baada ya kocha wake, Ally Bizimungu kutua na nyota wawili kutoka Nigeria na Ghana na wote wanajua kufunga mabao unaambiwa.
Kocha huyo aliyekuwa katika mapumziko mafupi kwao nchini Rwanda alitua juzi Alhamisi akiwa na nyota hao tayari kwa kuanza kazi klabuni hapo.
Waliotua ni washambuliaji Mnigeria Edwine Edwine na Mghana Atu Joseph wamekuja kwa lengo la kuhakikisha Mwadui inakuwa tishio msimu ujao.
Bizimungu alisema kuwa nyota hao wamesaini kandarasi ya mwaka mmoja kila mmoja, tayari wameshaungana na wenzao wakiendelea kujifua.
Alisema kuwa malengo yao yalikuwa ni kusajili nyota sita, ambapo hadi sasa wameshafika watano wakiwamo waliopandishwa kutoka kikosi B.
“Tulihitaji kuongeza wachezaji sita na bahati nzuri watano tumeshamalizana nao wanaendelea kujifua wakati tukiendelea kusaka nafasi ya huyo mmoja ambaye nataka awe mkali,” alisema Bizimungu.
Kocha huyo Mnyarwanda aliongeza kuwa kabla ya Ligi Kuu kuanza anahitaji vijana wake wawe fiti na kwamba mazoezi anayowapa lazima timu pinzani ziumie.
“Hakuna kulala mazoezi ni mwanzo mwisho,nataka Ligi ikianza tusiwe na vikwazo vyovyote nitahakikisha kila mchezaji anakuwa fiti ili kufikia malengo yetu”alisema Mnyarwanda huyo.