Kocha Maxime mzuka umepanda unaambiwa

Muktasari:

  • Kagera katika mechi mbili walizocheza nyumbani imefungwa 2-1 na Mwadui na kutoka suluhu na African Lyon hivyo anakwenda Musoma kwa lengo moja tu kushinda dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Karume Musoma.

Mwanza. Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ameangalia mwenendo wa kikosi chake katika mechi mbili zilizopita na kutamba kupata pointi tatu dhidi ya Biashara United.

Kagera katika mechi mbili walizocheza nyumbani imefungwa 2-1 na Mwadui na kutoka suluhu na African Lyon hivyo anakwenda Musoma kwa lengo moja tu kushinda dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Karume Musoma.

 Kocha Maxime alisema kwa jinsi wachezaji wake walivyoanza ligi wameonyesha kiwango ambacho ni dhahiri mchezo wao na Biashara kuna uwezekano mkubwa wa kuvuna pointi tatu.

Alisema licha ya kujiamini, lakini wataenda kwa tahadhari kubwa katika kuwavaa wapinzani hao na kusema kuwa amewaandaa vyema nyota wake kuhakikisha hawafanyi makosa ambayo yanaweza kuwagharimu.

“Wachezaji wako vizuri na kwa mechi mbili tulizocheza nimefurahi kwa kiwango walichoonyesha, kikubwa tunaenda ugenini kuwakabiri Biashara kwa tahadhari kwa lengo la kusaka ushindi,”alisema Maxime.

Kocha huyo aliongeza kuwa katika kikosi chake hakuna majeruhi wala mchezaji anayeweza kukosa mchezo huo kwa sababu yoyoye isipokuwa wanasubiri siku ifike ili benchi la Ufundi liamue nani wa kucheza.

Alisema kuwa licha ya ushindani uliopo lakini mpango wao ni kujiandaa kwa mechi zote kuhakikisha wanashinda ili kumaliza Ligi wakiwa nafasi nzuri na kwamba wana kikosi kipana ambacho kinaweza kubadili matokeo wakati wowote.