Kocha Matola kamaliza kazi yake Lipuli mapema tu

KOCHA wa Lipuli ya Iringa, Selemani Matola, mjanja sana kwani amemaliza mapema tu kazi ya kuunda kikosi chake cha msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, kisha kuwaachia mabosi wake wamalizane na wachezaji aliowataka.

Matola amesema amepata wachezaji 10 kati ya wengi waliojitokeza kufanya majaribio ndani ya kikosi hicho na majina yao ameyakabidhi kwa uongozi.

Lipuli iliyopiga kambi jijini Dar es Salaam na ikipiga tizi Uwanja wa Karume, ni kati ya timu tatu zilizopanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao na kwa mujibu wa Matola ni kwamba wachezaji hao 10 bado hawajasaini.

“Tayari nimefanya kazi yangu ya kuwaangalia wachezaji walioniletea kuwajaribu, nimewaona 10 wanaonifaa na jukumu lililobaki lipo kwa viongozi wawasainishe kisha wakabidhiwe kwangu tena,” alisema Kocha Matola.

Kocha huyo alisema licha ya kusubiri wachezaji hao wapya kusainishwa ili kuungana na wengine, benchi lao linaendelea na maandalizi ya mechi yao ya kufungua msimu dhidi ya Yanga itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Agosti 27.

Meneja wa timu hiyo, Mrisho Selemani, alisema mipango yao ya kuweka kambi Dar es Salaam ni kuhakikisha wanacheza mechi nyingi na kwa kuanza watavaana na Kagera Sugar wikiendi hii kabla ya kuwavaa Mbeya City, Azam na wakali wazoefu wengine wa Ligi Kuu ili kupima makali ya silaha zao.