Kocha JKT Ruvu atamba kurejea Ligi kuu

Wednesday September 13 2017

 

By Oliver Albert

Kocha mkuu wa JKT Ruvu, Bakari Shime amesema wapo tayari kwa ajili ya Ligi Daraja la Kwanza itakayoanza Jumamosi  huku wakiwa na malengo ya kurejea Ligi Kuu Bara kwa kishindo.

JKT iliyoshuka daraja msimu uliopita  itaanza harakati zake za kurejea Ligi Kuu kwa kupambana na maafande wenzao wa Mgambo JKT , Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Shime alisema wamefanya maandalizi mazuri  kuelekea mchezo huo na kwa ajili ya ligi nzima ili kuhakikisha wanarejea tena kwa kishindo kwenye Ligi Kuu.

"Tulianza maandalizi muda mrefu na nina kikosi imara ambacho najua kitatoa ushindani na pia  kitatimiza malengo tuliyojiwekea kuhakikisha tunarejea tena ligi kuu.

"Najua ligi daraja la kwanza ni ngumu lakini tumejipanga kukabiliana na timu yoyote pia tumeweka malengo ya kupata ushindi kwenye uwanja wowote iwe ugenini au nyumbani"alisema Shime.

Naye msemaji wa JKT Ruvu,Afisa mteule Daraja la Pili, Costantine Masanja alisema timu hiyo itatumia uwanja wa Mbweni JKT kama uwanja wake wa nyumbani kwenye ligi hiyo.

Alisema wakati wowote kuanzia sasa JKT Ruvu itasafiri kwenda Tanga tayari kuikabili Mgambo JKT katika mechi ya ufunguzi wa ligi.