Kocha Emery akatisha likizo ya Ozil

Mesut Ozil

Muktasari:

  • Supastaa Mesut Ozil ameamua kukatisha mapumziko yake na kurudi Arsenal fasta baada ya wachezaji wenzake kumwaambia utamu wa mazoezi ya Emery, ambaye kwa sasa ametua kwenye kikosi hicho kuchukua mikoba ya Arsene Wenger, aliyeng'atuka mwishoni mwa msimu uliopita.

LONDON, ENGLAND. MAMBO ya Unai Emery huko Arsenal si mchezo unaambiwa.

Supastaa Mesut Ozil ameamua kukatisha mapumziko yake na kurudi Arsenal fasta baada ya wachezaji wenzake kumwaambia utamu wa mazoezi ya Emery, ambaye kwa sasa ametua kwenye kikosi hicho kuchukua mikoba ya Arsene Wenger, aliyeng'atuka mwishoni mwa msimu uliopita.

Ozil alikuwa kwenye kikosi cha Ujerumani wakati wa fainali za Kombe la Dnia 2018 huko Russia na amekuwa akibebeshwa lawama tu baada ya timu hiyo kuboronga na kushindwa kuvuka hatua ya makundi licha ya kwamba walikuwa mabingwa watetezi.

Ozil alicheza hovyo kwelikweli katika mechi ya kwanza ya kichapo kutoka kwa Mexico, akapigwa mkeka kwenye mechi ya pili na timu ikashinda dhidi ya Sweden, lakini aliporudishwa kikosini kwenye mechi ya tatu, Ujerumani wakafungwa tena, safari hii walichapwa na Korea Kusini. Baba yake alimshauri ang'atuke kuichezea timu ya taifa.

Mastaa wa Arsenal kwa sasa wapo kwenye mazoezi makali kweli kweli, Emery akijaribu kuwaweka fiti wachezaji wake kabla ya mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu England ambapo watamenyana na mabingwa, Manchester City.

Taarifa zinadai kwamba Ozil alikuwa akiwasiliana na wachezaji wenzake wa Arsenal na kuambiwa kuhusu utaratibu mpya wa mazoezi kwenye kikosi chao kwa sasa na kumfanya aamue kukatisha likizo yake ili kurudi kuungana na wenzake. Msimu ujao, Ozil ataonekana akiwa na jezi Namba 10, kitu ambacho alikuwa akikitamani tangu aliposajili mwaka 2013. Namba hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Jack Wilshere.