Kocha Bilo afikiri pointi tatu kwa Singida United

Dar es Salaam. Kocha msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal 'Bilo' amesema anatambua kazi kubwa iliyo mbele yao na  wanataka kuhakikisha wanapata pointi tatu za kwanza dhidi ya Singida United Jumamosi.

Stand United imepoteza michezo yote miwili iliyocheza mpaka sasa, dhidi ya Mtibwa Sugar 1-0  na Lipuli 1-0  na Jumamosi itaikabili timu tajiri ya Singida United kwenye Uwanja wa Kambarage Shiyanga.

Bilo anaamini kuwa walipoteza mechi kutokana na wachezaji wake wengi kukosa uzoefu wa mashindano na pia kucheza ugenini lakini sasa wanarejea nyumbani hivyo watapata nguvu kubwa kutoka kwa mashabiki wao itakayowasaidia kupata ushindi wao wa kwanza msimu huu.

Alisema anajua ujio Singida United  kwenye Ligi Kuu Bara ulikuwa wa kutikisa kutokana na usajili iliofanya lakini hawana hofu nayo sana kwani imeonekana kuwa bado haijakaa sawa kutokana na kukosa muunganiko wa wachezaji wake.

"Tulianza ligi kwa kuyumba lakini yote ilitokana na kwamba tuna wachezaji wengi wapya kikosini tena wasio na uzoefu wa ligi lakini muda si mrefu watakaa sawa na mambo yataanza kutunyookea.

"Tunaendelea na maandalizi yetu ya kuikabili Singida United, kitu ninachojivunia ni kwamba tutakuwa nyumbani, mbele ya mashabiki wetu ambao wamekuwa wakitupa sapoti kubwa na nina uhakika mechi hiyo tutapata ushindi wetu wa kwanza msimu huu," alisema Bilo.

Aliongeza, "Singida sio timu mbaya kwani imesajili wachezaji wengi wazuri wenye majina lakini ukiangalia bado nayo inahangaika kutafuta muunganiko wa wachezaji wake kama sisi, hivyo sina hofu nayo. Tumejiandaa kupambana nayo na kushinda mchezo huo.”