Klabu 12 kuchuana kuogelea Taifa leo

Muktasari:

Wenyeji Dar es Salaam itawakilishwa na klabu za Blue Fins, Champion Rise, Dar Swim na Taliss.

 

Dar es Salaam.MAMBO ni moto!! Ndivyo itakayokuwa kwenye mashindano ya taifa ya kuogelea yanayofanyika leo na kesho kwenye bwawa la kuogelea la shule ya kimataifa ya Tanganyika (IST), Dar es Salaam.

Klab 12 zenye wachezaji 150 zitachuana kwenye mashindano hayo yatakayoshirikisha waogeleaji kutokana mikoa mbalimbali nchini.

Wenyeji Dar es Salaam itawakilishwa na klabu za Blue Fins, Champion Rise, Dar Swim na Taliss.

Arusha yenyewe itakuwa na uwakilishi wa klabu ya Shule ya Braeburn huku Kilimanjaro yenyewe itawakilishwa na shule ya kimataifa Moshi.

Zanzibar yenyewe imetuma 'jeshi' kutoka klabu ya Wahoo, KMKM, na JKU  wakati Mwanza itang'arishwa na Mwanza Swim  na Morogoro yenyewe itakuwa na uwakilishi wa shule ya Kimataifa ya Morogoro (MIS).

Kocha Alex Mwaipasi alisema mashindano hayo yatasimamiwa na jopo la makocha waliobobea na kusisitiza kuwa mabingwa wataondoka na zawadi mbalimbali ikiwamo vikombe.