Kizungumkuti

Muktasari:

  • Juventus ilitua jijini Madrid ikihitaji kurudisha mabao matatu ambayo ilichapwa jijini Turin wiki moja iliyopita, na kweli mpaka kufikia dakika ya 90 ilikuwa imerudisha mabao yote matatu. Lakini ghafla, Mwamuzi wa Kiingereza, Michael Oliver akaizawadia penalti Real Madrid na hivyo kuipa nafasi ya kutinga nusu fainali.

MADRID, HISPANIA

BAADA ya usiku wa kushangaza wa Jumanne, juzi Jumatano usiku kulikuwa na usiku mwingine wa ajabu katika pambano la Ligi ya Mabingwa. Ilikuwa kama filamu ya kusisimua ambayo mtunzi wake anastahili sifa.

Juventus ilitua jijini Madrid ikihitaji kurudisha mabao matatu ambayo ilichapwa jijini Turin wiki moja iliyopita, na kweli mpaka kufikia dakika ya 90 ilikuwa imerudisha mabao yote matatu. Lakini ghafla, Mwamuzi wa Kiingereza, Michael Oliver akaizawadia penalti Real Madrid na hivyo kuipa nafasi ya kutinga nusu fainali.

Beki wa Juventus, Mehdi Benatia, ambaye ni staa wa kimataifa wa Morocco alionekana kumsukuma kwa nyuma mshambuliaji wa Madrid, Lucas Vázquez na Mwamuzi Oliver alipoamuru penalti, Cristiano Ronaldo hakufanya makosa.

Kabla ya Ronaldo kupiga penalti hiyo, Mwamuzi Oliver alimpa kadi nyekundu kipa mkongwe, Gianluigi Buffon na hiyo ni mechi yake ya mwisho katika historia ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa sababu atastaafu mwishoni mwa msimu.

Na sasa kipa huyo mwenye umri wa miaka 40 amemwaga maneno mazito ya hasira dhidi ya Mwamuzi Michael Oliver akimshutumu kwa kuibeba Real Madrid katika pambano hilo.

“Najua mwamuzi aliona, ilikuwa ni penalti ya kijinga. Lilikuwa tukio la kijinga na tulinyimwa penalti ya wazi katika mchezo wa kwanza, hauwezi kutoa penalti kama hii. Timu ilitoa kila ilichonacho lakini mwanadamu wa kawaida hawezi kuharibu ndoto zenu wakati mnatazamiwa kuweka historia kubwa,” alisema Buffon kwa hasira.

“Ni wazi kwamba hawezi kuwa na moyo kifuani kwake. Ana pipa la takataka. Juu ya yote kama hauna ubavu wa kutembea katika uwanja kama huu na kuchezesha, inabidi ukae jukwaani na mke wako na watoto mkinywa Sprite na kula viazi. Hauwezi kuhitimisha ndoto za timu kama hivi,” alisema Buffon.

“Unahitaji kuwa muuaji kuruhusu maamuzi mawili ya mwisho ambayo mwamuzi aliyafanya,” aliongeza kipa huyo ambaye hata hivyo, alikiri kwa jumla wa mechi zote mbili Madrid ilistahili kusonga mbele.

“Real Madrid ilistahili kusonga mbele kwa kuangalia mechi zote mbili. Nawatakia kila la kheri na siku zote imekuwa heshima kubwa kwangu kucheza dhidi ya klabu hii, lakini kimsingi tulipaswa kwenda nayo hadi dakika za nyongeza,” alisema Buffon.

Hata hivyo, Vazquez mwenyewe anaamini ile ilikuwa penalti ya wazi na haoni sababu kwanini Juventus ililalamika sana kwa maamuzi ya mwamuzi, Michael Oliver.

“Ile ilikuwa penalti? Ndio. Cristiano alipiga mpira kichwa kuja kwangu nikiwa karibu na lango na nilikuwa nakaribia kumalizia. Beki wa kati alikuja mgongoni kwangu na kunigonga. Hakuna swali kuhusu hilo. Juve inapinga? Ni kitu cha kawaida. Ilikuwa ni dakika ya mwisho. Leo inabidi liwe funzo kwetu,” alisema staa huyo.

Hata hivyo, staa wa zamani wa Juventus, Alessandro Del Piero ambaye alicheza sambamba na Buffon katika klabu ya Juventus kwa miaka mingi amedai kushangazwa na madai ya kipa huyo huku akiamini alisema hivyo kwa sababu ya hasira.

“‘Wakati Gigi anapomuongelea mwamuzi inakuwa ngumu kuamini. Sielewi kwanini aliingize pambano lililopita, hivi ndivyo mpira ulivyo na unajaribu kuchambua mambo ya sasa kama ni mabaya au mazuri. Nadhani baada ya siku chache ataongea vitu tofauti kuhusu mwamuzi kuliko alichosema sasa,” alisema Del Piero.