Kiyombo aichapa KMC nyumbani

Muktasari:

Kiyombo amecheza mechi yake ya kwanza Singida United baada ya kutoka katika majaribio Afrika Kusini

Dar es Salaam. Mechi ya kwanza nyumbani kwa KMC imekuwa na nuksi baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Singida United kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.

Kabla ya mchezo wa leo, KMC ilicheza mechi tatu mfululizo ugenini dhidi ya timu za JKT Tanzania, Ruvu Shooting na Coastal Union ambazo zote ilitoka sare na kujikusanyia pointi tatu.

Bao pekee lililoizamisha KMC leo, lilifungwa na Habib Kiyombo katika kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa baada ya beki wa KMC, Ally Msengi kumfanyia madhambi Geofrey Mwashiuya.

Kuingia kwa bao hilo kuliiamsha KMC ambayo ilianza kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Singida, lakini washambuliaji wake walikosa umakini wa kutumia nafasi.

Kipindi cha pili KMC waliendelea lulishambulia bao la Singida United kama nyuki, lakini safu ya ulinzi ya wapinzani wao ilikuwa makini kuondosha hatari zote zilizoelekezwa golini kwao.

KMC wanapaswa kujilaumu wenyewe baada ya mshambuliaji wao Emmanuel Mvuyekure kupaisha penalti dakika ya 49 iliyotolewa baada ya Kenny Ally kunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Licha ya timu zote mbili kufanya mabadiliko kipindi cha pili, matokeo hayakuweza kubadilika.

Singida iliwatoa Hans Kwofee, Geofrey Mwashiuya na Habib Kiyombo huku nafasi zao zikichukuliwa na Awesu Awesu, Lubinda Mundia na Eliuter Mpepo wakati KMC iliwatoa Cliff Buyoya na Bryson Rafael huku nafasi zao wakiingia Samiru Mohammed na Omary Ramadhan.