Kiwango cha Liverpool chamkuna Klopp

Muktasari:

  • Akizungumzia mchezo huo na namna anavyoiona Ligi kwa ujumla, Klopp alisema kuwa amestaajabu ubora wa kikosi chake kwani hakutarajia kuiona katika kiwango bora kama hicho.

London, England. Baada ya kuanza Ligi Kuu England kwa kishindo ikiitandika kwa mabao 4-0, West Ham United, Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amefunguka na kusema timu hiyo ni bora zaidi ya alivyodhani.
Akizungumzia mchezo huo na namna anavyoiona Ligi kwa ujumla, Klopp alisema kuwa amestaajabu ubora wa kikosi chake kwani hakutarajia kuiona katika kiwango bora kama hicho.
Alisema hazungumzi hivyo kwa sababu ya ushindi bali tathmini ya mchezo ndiyo iliyomstaajabisha, kutokana na timu hiyo kumiliki mpira kwa kiwango cha juu.
Katika mchezo huo, mabao ya Liverpool yaliwekwa kimiani na Mohammed Salah, dakika ya 19 na Sadio Mane dakika ya 45 na kwenda mapumziko wakiongoza.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Liverpool walijipatia bao la tatu likifungwa na Mane tena na Daniel Sturridge akahitimisha karamu hiyo ya mabao zikiwa zimesalia dakika mbili mchezo kumalizika.
“Kwa kweli nimestaajabishwa na kiwango chetu, sikutarajia kuwa timu Ipo katika kiwango bora namna hii, kila mchezaji alitimiza wajibu wake kwa kiwango cha juu,” alisema.
Alisema timu inapoanza Ligi kwa ushindi inakuwa na nafasi nzuri ya kufanya vizuri katika mechi nyingi zinazofuata kutokana na wachezaji kujiamini.
Liverpool ambayo ilianza Ligi ikiwa nyumbani kwenye uwanja wake wa Anfield, wikiendi hii itasafiri kuifuata Crystal Palace, kabla ya kuikaribisha Brighton katika mzunguko wa tatu wa Ligi hiyo.