Kiungo wa Simba

Muktasari:

  • Taarifa ni kwamba pesa zilizomzuia kiungo huyo aliyesainishwa mkataba wa miaka miwili kutoka Mtibwa Sugar, ni Sh 25 milioni, ambazo zinapaswa kutolewa kule kambi ya Manungu.

SIMBA imeshatua nchini Uturuki tayari kuweka kambi wakijiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, hata hivyo habari mbaya ni kwamba kiungo wao mpya Hassan Dilunga amezuiwa kuambaa na msafara huo kisa kikiwa ni mkwanja tu.

Taarifa ni kwamba pesa zilizomzuia kiungo huyo aliyesainishwa mkataba wa miaka miwili kutoka Mtibwa Sugar, ni Sh 25 milioni, ambazo zinapaswa kutolewa kule kambi ya Manungu.

Ipo hivi; Simba imepaa alfajiri ya jana Jumapili kuelekea Uturuki na tayari imeshatua katika kambi ya zaidi ya wiki mbili, lakini jina la Dilunga halikuwa miongoni mwa nyota waliosafiri.

Mabosi wapya wa Dilunga (Simba) wanatakiwa kulipa mpunga huo kule Mtibwa ili kuvunja mkataba wa mwaka mmoja uliosalia kwao.

Mtu wa karibu ndani ya Mtibwa, aliliambia Mwanaspoti kuwa Simba ilishamalizana na Dilunga, ila imepata ugumu kumalizana na mabosi wa Mtibwa wanaotaka walipwe Sh 25 milioni.

“Mtibwa inataka fedha hizo, lakini Simba inataka kutoa Sh 20 milioni, ndio maana imekuwa vuta nikuvute. Dilunga kaachwa kwenye msafara kwa sababu Simba hawataki kuingia matatani na TFF mbele ya safari.”

“Kama Simba itaamua kumalizana na mabosi wa Manungu, jamaa hata kesho anaweza kuondoka kwa sababu hawana tatizo naye ila wanataka kumaliziwa chao,” kilisema chanzo hicho makini.

Naye Diluinga alipoulizwa ishu hiyo, alisema anasubiri mabosi wake wamalizane ili aweze kutoa kauli kwani amebaki njia panda.

“Siwezi kusema chochote kwani suala hili lipo chini ya meneja wangu, lakini nilipoongea naye na hata viongozi wangu wa Mtibwa wananiambia wapo hatua nzuri kumalizana,” alisema.

Mkurugenzi wa Mtibwa, Jamal Bayser simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa, na hakukuwa na kiongozi wa Simba aliyepatikana kufafanua ishu hiyo.

Mbali na Dilunga nyota wengine wa Simba waliobaki nchini huku wengine wakipaa Uturuki ni Erasto Nyoni mwenye matatizo ya kifamilia inaelezwa ataondoka Jumatano hii.

Pia wamo Ally Shomari, Jamal Mwambeleko, makipa Emmanuel Mseja na Said Mohammed na straika chipukizi, Moses Kitandu walio mbioni kutolewa kwa mkopo. Naye Said Ndemla akikwama kwa vile hajamalizana na Simba katika kusaini mkataba mpya.

Ndemla alisema kama mambo yatakwenda sawa huenda akapaa sambamba na Nyoni kuelekea kambini keshokutwa Jumatano .