Kiungo aikataa Simba aenda zake Yanga

Tuesday July 11 2017

 

By MWANAHIBA RICHARD

SIMBA hii haitamuacha mtu salama. Mabosi wapya wa Simba hawataki utani na kwa kuonyesha kwamba wako kazini, wamepiga simu Mbeya City kuulizia watani zao Yanga wamefikia wapi katika uhamisho wa kiungo, Raphael Daudi, kisha kuweka ofa yao mezani.

Lakini Meneja wa mchezaji huyo amewaambia Simba; “No, atacheza Yanga.”

Yanga tayari imefikia makubaliano ya kumpa mkataba wa miaka miwili kiungo huyo fundi aliyekuwa na Taifa Stars kule Afrika Kusini, lakini hajasaini. Juzi Jumapili Simba waliingilia usajili huo ambapo walipiga simu kwa meneja wa mchezaji huyo kwa nia ya kutaka kumsajili, lakini akawatolea nje.

Mwanaspoti linafahamu kuwa kigogo mmoja wa Simba juzi alikuwa akihaha jinsi ya kumalizana na Raphael ili asitue Jangwani, lakini hakufanikiwa baada ya mchezaji huyo kumpa maelekezo ya kwamba awasiliane na meneja wake ingawa alifanya mawasiliano hayo na kuambiwa kuwa asubiri kwanza mchezaji amalizane na majukumu ya timu ya Taifa.

Mwanaspoti lilimtafuta Meneja wa mchezaji huyo, Beda Morris, ambaye alikiri kupigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni kiongozi wa Simba ambaye alielezea nia yake ya kumhitaji Raphael.

“Kuna kiongozi Simba (anamtaja jina) alinipigia simu akihitaji huduma ya Raphael ila nimemwambia asubiri kidogo mchezaji ana majukumu na timu ya Taifa. Ofa yao haina tofauti na ya Yanga,” alisema Morris.

“Mpaka sasa tunawapa Yanga nafasi kubwa zaidi kwani pamoja na fedha, tunatazama nafasi yake ya kucheza. Akienda Simba hataweza kucheza kama tunavyotaka kwani pale kuna wachezaji wengi wa nafasi yake tofauti na Yanga ambapo tuna uhakika atacheza, hivyo asilimia za kwenda Simba ni 20 tu.”

Kuhusu usajili, kuna habari pia kuwa  vigogo wa Simba wanatafuta namna ya kumnasa kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ aliye Afrika Kusini akijaribiwa na klabu ya Pretorial University.

Wakati huohuo, Yanga jana iliendelea kuwapima afya wachezaji wake na vipimo hivyo vilimpasisha straika Ibrahimu Ajibu kuwa yupo fiti kukipiga.

 Ajibu ametua Jangwani akitokea Simba.