Kiukweli, hakuna haja ya kumuhurumia Conte

Muktasari:

Kuna wanadamu wanalala nje na hawana uhakika wa kula.

KUNA watu wanahitaji huruma kutoka kwa wanadamu wengine. Kuna watoto wapo Syria hawana makazi, hawana wazazi, wamezingirwa na risasi.

Kuna wanadamu wanalala nje na hawana uhakika wa kula.

Kuna wanadamu wanahitaji huruma ya wanadamu wengine.

Wapo wengi lakini sio Antonio Conte. Huyu kocha wa Chelsea. Kwa nini nimuhurumie? Naweza kupeleka huruma yangu kwa wanadamu wengine lakini sio kwa Conte na matokeo yake mabovu msimu huu. Aliyetaka mwenyewe.

Conte alitolewa Kombe la Ligi na mgonjwa mwenzake, Arsene Wenger. Katika msimamo wa ligi hana uhakika wa kuingia Top Four. Amebaki katika michuano ya FA lakini hatujui safari yake itaishia wapi ingawa namtakia kila la kheri.

Katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya alitolewa na Barcelona. Katika lugha nyingine alitolewa na Lionel Messi. Katika mechi mbili Messi alihusika katika mabao manne ya Chelsea. Alifunga matatu na kupika moja la Ousmane Dembele.

Katika pambano hili la pili ambalo Chelsea ilitolewa, Conte alionekana akimfuata Messi na kutabasamu huku akimsifu kwa ubora wake uliomtupa nje. Sawa, hakuna shida kumsifu Messi, lakini kama angekuwa na akili ya kutabasamu mbele ya Diego Costa na Nemanja Matic mwishoni mwa msimu uliopita si ajabu Chelsea isingefika hapa. Alitumia akili gani kuachana na Diego Costa. Huyu ni mchanganyiko wa washambuliaji wa kizamani na wa sasa. Mashabiki wote ambao sio wa Chelsea walikuwa wanamchukia Diego kwa sababu alikuwa hatari, ana nguvu halafu mkorofi. Hakuna ambaye hakupenda kuwa na Diego katika timu yake.

Pamoja na utukutu wake wote, Costa ni hatari mno. Costa ni mchezaji wa mechi kubwa na ndogo. Costa ndiye aliyempa ubingwa katika msimu wake wa kwanza alipowasili klabuni hapo akitokea Italia. Jaribu kukumbuka kombinesheni ya Costa na Cesc Fabregas. Jaribu kukumbuka kombinesheni ya Costa na Eden Hazard.

Mbaya zaidi unamtoa Costa halafu unamleta mtu mlaini kama Alvaro Morata. Kama katika kikosi chako unamuondoa Costa, basi labda umnunue Sergio Aguero au Luis Suarez ambao wamewahi kuthibitisha ubora wao katika Ligi Kuu ya England.

Inawezekana Costa alikuwa mkorofi lakini wakati mwingine kocha bora ni yule anayeweza kudumu na wachezaji wakorofi klabuni. Ni kama Sir Alex Ferguson alivyomvumilia Roy Keane mpaka mpira ulipoisha miguuni ndipo akamruhusu apeleke ukorofi wake Celtic.

Kuna wachezaji wa aina ya Costa ambao wakati mwingine unalazimika kuwavumilia kwa sababu mwisho wa siku uwanjani wanakupa unachotaka. Leo jiulize kama mshambuliaji wa Chelsea ambaye amefikia nusu ya mabao ya Costa msimu uliopita.

Halafu kuna hili suala la kumtoa Nemanja Matic. Unaachana vipi na Matic katika timu yako kijingajinga tu kwa sababu ya Tiemoue Bakayoko ambaye alikuwa katika msimu wake wa kwanza Ligi Kuu ya England? Matic anakaba, anatawanya mipira, anapiga pasi ndefu na fupi. Unaachana vipi na Matic?

Bakayoko alikuwa hajawahi kugusa Ligi Kuu ya England. Leo muda mwingi anakaa benchi wakati Matic anawasha moto katika kikosi cha Jose Mourinho pale Old Trafford. Zaidi ya yote alipatikana kwa bei ya chini kabisa. Hata kumpiga benchi muda mwingi, David Luiz ni kosa jingine la kijinga. Kumruhusu Michy Batshuayi na kwenda kutafuta mshambuliaji mwingine ni kosa jingine la kijinga. Kila alipompa nafasi Batshuayi alikuwa anafunga lakini bado mechi ijayo angemuweka benchi.

Conte sio mtu wa kuhurumiwa. Alitumia wachezaji wengi aliowakuta klabuni hapo wakiwa wameshanunuliwa na wenzake, baada ya hapo akaanza kuwadharau akidhani ingekuwa rahisi kupata wachezaji mbadala wa mastaa hao.

Alitaka kuitengeneza timu yake lakini imeshindikana. Zaidi ya yote Conte alipaswa kutumia akili ya kawaida kuepuka makosa ambayo yalifanywa na Jose Mourinho na Claudio Ranieri ambao walichukua ubingwa kabla yake kwa misimu miwili iliyopita. Wote walifanya kosa ya kuvurugana na wachezaji wao katika vyumba vya kubadilishia nguo.

Mourinho baada ya kutwaa ubingwa na Chelsea akaanza kuvurugana na kina Costa, Hazard na wengineo. Akaishia kufukuzwa Desemba.

Ranieri akiwa na Leicester naye aliingia katika mkumbo huohuo wa kukorofishana na kina Kaspar Schameichel, Jamie Vardy na wengineo. Na yeye akafukuzwa wakati msimu ukiwa njiani.

Conte alipaswa kulikwepa jinamizi hili ambalo sijui kwanini kwa sasa linasumbua katika Ligi Kuu ya England, lakini yeye bado akaingia katika mkumbo huohuo.

Jenerali hawezi kwenda vitani akiwa amebwatukiana na mabrigedia wake. Hii haipo popote pale.