Kitakachowakuta Yanga mechi ya ufunguzi hiki hapa

KOCHA wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila mjanja sana, amesema wanahitaji kuanza kwa kishindo katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga kwa kuamini kuwa hiyo ndio mechi ya kuianzisha safari yao ya ubingwa.
Hata hivyo Katwila alisema hawataivaa Yanga kizembe kwa kuamini eti ni wachovu kwa kelele kwamba inatafunwa na ukata mkali, badala yake wataivaa kininja ili kupata ushindi katika mechi hiyo italayopigwa Agosti 22.
"Kama kuna kitu huwa nasisitiza wachezaji wangu ni juu ya nidhamu kwa mchezo na kila dakika wanapokuwa uwanjani, nikiamini hilo ndilo jambo pekee linaloweza kuwafikisha mbali.
"Mambo ya Yanga nawaachia Wanayanga wenyewe, nawaandaa kikamilifu nyota wangu kwa kila mchezo kama fainali bila kuibeza timu yoyote," alisema.
"Mtibwa Sugar kwa sasa tuna mashindano ya Shirikisho Afrika, unategemea usipowafunda wachezaji wako kuzingatia nidhamu nini kinafuata, tunahitaji kuonyesha kitu cha tofauti katika anga hizo pamoja na kwenye ligi kuu," alisema.