Kisiga hataki kiki

KIUNGO mkongwe, Shaban Kisiga ametamba anajua mpira ndiyo maana hana muda wa kushoboka na kuuza sura kwa klabu kongwe Simba na Yanga ili asajiliwe.

Alifafanua kauli yake, kwamba anachokifanya yeye ni kuonyesha burudani uwanjani na wala sio kiki za nje ya kazi yake kama wanavyofanya wachezaji wengine.

“Ifikie hatua wachezaji tusikubali kwenda na upepo wa siasa za mpira badala yake, tuheshimike kutokana na viwango vyetu, hilo litatujengea kuheshimika kwenye klabu tunazozitumikia,” alisema.

Alisema amejifunza kitu kwenye ujio wa kiungo wa kimataifa, Mkenya Victor Wanyama, anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Tottenham Hotspurs ya England kuwa, licha ya kuja kwenye mapumziko lakini ametikisa Tanzania.

“Ikumbukwe kwamba alikuja kwenye mapumziko, lakini akadakwa.

Angalia jinsi ambavyo ameacha gumzo mtaani, licha ya kwamba kaondoka. Hilo ndilo tunalotakiwa kulifanya wachezaji na kuacha kushikwa akili zetu na watu wachache,” alisema