Kisa ishu ya Simbu! Riadha yagawanyika

Muktasari:

Mkwanja huo ambao ni Sh18 milioni, Class aliupata baada ya kushinda ubingwa wa dunia wa GBC kwa kumpiga Msauzi, Koos Sibiya, sasa unaambiwa upande wa pili kule kwenye riadha wakaibuka na hoja eti mbona kwa Simbu haikuwa hivyo?

WADAU wa Riadha wamelianzisha tena huku chanzo kikiwa ni Mwanariadha, Alphonce Simbu na mkwanja ambao Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alimkabidhi bondia Ibrahim Class hivi karibuni.

Mkwanja huo ambao ni Sh18 milioni, Class aliupata baada ya kushinda ubingwa wa dunia wa GBC kwa kumpiga Msauzi, Koos Sibiya, sasa unaambiwa upande wa pili kule kwenye riadha wakaibuka na hoja eti mbona kwa Simbu haikuwa hivyo?

Hoja hiyo ikaanza kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na katika kundi la whatsapp la riadha mpya huku kwa siku mbili mfululizo mjadala ukiwa ni Class, Simbu na hamasa ya serikali kwenye ngumi na riadha.

Mjadala si ukaenda mbali zaidi, unaambiwa mmoja wa wadau wa riadha akaibuka na hoja kwamba Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) halikumhamasisha Waziri Mwakyembe kuwasapoti wakati timu yao ikijiandaa na mashindano ya dunia ya Agosti kule Uingereza ambayo Simbu alileta medali ya shaba ya marathoni.

Mabishano yakaendelea zaidi kwa mdau mwingine kuibuka na kuitetea RT kwamba ilitekeleza wajibu wake na ndiyo sababu timu ilikabidhiwa bendera na waziri lakini kitendo cha kutoa fedha kwa Class na Simbu kutopewa hiyo ni ishu nyingine.

Ila Simbu mwenyewe wala hana hata habari ila anasema kuna maneno ameyasikia kwamba eti kutaka kwake kujitoa kwenye michezo ya madola ya Aprili kule Australia kuna watu wamezusha chanzo ni kutopewa chochote na waziri baada ya kushinda medali ya shaba ya dunia.

“Mengi yamezungumzwa lakini sio kweli, kuna watu waliwahi kunisimamisha barabarani hata siwafahamu wakaanza kunihoji kuhusu kujitoa kwenye madola , tena nasikia wengine wanasema eti sababu sikupewa chochote na waziri.

“Wala sio kweli na chanzo cha kuomba nisiwe kwenye timu hakikuwa hicho, nilikuwa na mtizamo mwingine kabisa ila ninayo mengi ya kuzungumza kuhusu riadha nasubiri wakati ufike tu niruhusiwe kufanya hivyo,” alisema mwanariadha huyo ambaye pia ni bingwa wa Mumbai Marathon na mshindi wa tano wa London Marathon.