Kisa Salah: Familia ya Ramos ilitishiwa maisha

Muktasari:

  • Ramos alisema katika fainali hiyo alimuumiza kwa bahati mbaya mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah, lakini mashabiki wa timu hiyo na wale wa Uingereza wamekuwa wakimtishia kupitia mitandano ya kijamii.

London, England. Nahodha wa Real Madrid na timu ya Taifa ya Hispania, Sergio Ramos amesema familia yake ilipokea vitisho baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka huu.

Ramos alisema katika fainali hiyo alimuumiza kwa bahati mbaya mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah, lakini mashabiki wa timu hiyo na wale wa Uingereza wamekuwa wakimtishia kupitia mitandano ya kijamii.

Beki huyo mwenye miaka 32, jana alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya mashabiki wa England kumzomea muda wote wa mchezo ambao Hispania ilishinda 2-1 dhidi ya wenyeji wao England kwenye Uwanja wa Wembley katika mashindano mapya ya Uefa Nations League.

"Suala la kuzomewa mimi haliniondoi mchezoni hata kidogo, lakini linakera kwa kiasi kikubwa na mwisho wa siku linakuumiza kisaikolojia,” alisema Ramos.

Alisema inasikitisha kuona watu wakikumbuka na kuzungumzia tukio hilo la mchezo wa fainali, lakini hawajadili wala kuzungumzia namna familia yangu hususani wanae wanavyopitia kipindi kigumu cha kutishiwa maisha.

Ramos alisema kwa anafahamu tabia za mashabiki wa Uingereza alijiandaa kisaikolojia kukabiliana na zomea zomea ambayo ingejitokeza ndiyo maana hakuathirika.

Mara kadhaa Mo Salah amekuwa akimshutumu Ramos kuwa alikusudia kumharibia maisha yake ya kisoka kwa kumchezea vibaya katika fainali ile.