Kiraka Stars abaki Mbao

Muktasari:

Kadito alisema anaona bora mchezaji wake aendelee kucheza katika kikosi cha Mbao kwasababu walimthamini na kumpa nafasi, tofauti na kipindi cha nyuma ambapo mchezaji huyo aliwahi kwenda Simba lakini walimtoa kwa kuona hana kiwango.

KIRAKA wa Taifa Stars, Boniphace Maganga ataendelea kucheza Mbao FC kwa msimu mpya wa mashindano baada ya Denis Kadito kuridhishwa na namna timu hiyo inavyomtumia na kumpa heshima nchini.
Kadito alisema anaona bora mchezaji wake aendelee kucheza katika kikosi cha Mbao kwasababu walimthamini na kumpa nafasi, tofauti na kipindi cha nyuma ambapo mchezaji huyo aliwahi kwenda Simba lakini walimtoa kwa kuona hana kiwango.
“Maganga aliwahi kucheza Simba lakini walimtoa baada ya kuona kuwa hana nafasi, lakini alipata nafasi Mbao na akacheza hadi anaitwa timu ya Taifa. Ni bora mchezaji wangu aendelee kucheza timu anayopata nafasi ya kuonekana na sio kwenda timu kubwa halafu hachezi,”alisema.
Kadito aliongeza kuwa haangalii sana pesa katika masuala ya usajili kwasababu mchezaji anayetakiwa kwenda kucheza nje ya nchi ni yule ambaye anapata nafasi katika timu yake.
“Sio kama sihitaji mchezaji wangu acheze vilabu vikubwa lakini naangalia kwanza anapoenda anaweza akapata nafasi ya kucheza?, ofa zipo zimekuja lakini yeye mwenyewe anahitaji kucheza na ukiwa unacheza hata ukitaka kuondoka thamani yako inakuwa ya juu tofauti na ukiwa benchi,” alisema.