Kipa wa Yanga aliamsha dude

YANGA ipo katika kipindi  kigumu cha kuyumba kiuchumi jambo linalodaiwa kuikwamisha kuwamalizia fedha za usajili baadhi ya wachezaji wake akiwemo kipa, Beno Kakolanya aliyesajiliwa kutoka Prisons.

Lakini kwa kipa huyo kuna taarifa pia kuwa iantokana na kushindwa kwake kufanya vyema ingawa maelezo mengine ni kwamba alikuwa anaumwa na hata mechi yao na Singida United bado alikuwa akisumbuliwa na malaria.

Meneja wa  mchezaji huyo, Selemani Haroub, ameliambia Mwanaspoti kuwa wiki hii watawasilisha barua rasmi katika klabu ya Yanga ili kudai madai hayo ya fedha yaliyobaki ambayo imeelezwa kwamba kwa utaratibu wa kawaida Yanga wamevunja mkataba wa Beno kwani wameenda kinyume na makubaliano yao.

Haroub alisema kuwa wanaitaka  Yanga kukamilisha mchakato huo ndani ya siku 14 na ikishindikana basi hatua zingine zitachukuliwa kama sheria na kanuni za usajili ziinavyoelekeza.

“Ni kweli tunawadai Yanga fedha ya usajili iliyobaki,  mara  kadhaa tumekuwa tukiwakumbusha kwa njia ya mdomo tukiamini kwamba watashughulikia ila imekuwa ngumu hivyo tunawaandikia barua rasmi na kuwapa muda walifanyie kazi,” alisema.

“Ukiangalia kanuni za usajili  tayari Yanga wamevunja mkataba wa Beno, kwani makubaliano yetu ya kumalizia hiyo pesa yamepita na tumewavumilia,  wakishindwa kumlipa kwa muda ambao tutakuwa tumewaelekeza tutakwenda TFF ili kama vipi mchezaji awe huru kabisa.”

Meneja huyo aliweka wazi kuwa alikubali Beno kutua Yanga ili apate mafanikio makubwa zaidi lakini anaona jambo hilo limekuwa tofauti.

“Kwa Beno sasa ni kama anarudi nyuma, ni kipa mzuri ila anakosa nafasi ya kuonyesha kiwango chake, nimezungumza naye na nimemshauri aendelee kupambana,” aliongeza.

Beno ana alisaini mkatana wa miaka miwili utakaomalizika Juni mwakani.