Kindoki awatibulia mastraika Yanga

KIPA mpya wa Yanga, Klaus Kindoki sio mtu wa mchezo mchezo jamaa ni mbishi akiwatibulia mastraika wake katika mazoezi ya timu hiyo akichomoa mashuti ya maana.

Kindoki ambaye amesajiliwa na Yanga msimu huu jamaa amekuja kufanya kazi na akiwa mazoezini utakubali kazi yake anavyofuta mabao ya wazi

Katika mazoezi ya juzi jioni na jana asubuhi Kindoki alianza kwa kutibua mabao ya wazi ya straika raia mwenzake wa DR Congo Heritier Makambo.

Kindoki aliokoa mabao mawili ya Makambo na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo kumshangilia huku wakiulaumu uongozi wao kwa kuchelewa kumsajili.

Mashabiki hao wa Yanga walionekana kuchukizwa wakisema kumbe viongozi wao wanawajua makipa wazuri lakini wakaamua kumleta Youthe Rostand.

Rostand amekuwa akilaumiwa na mashabiki wa timu hiyo kuwa kiwango chake si cha kuridhishwa kwani amekuwa akifungwa magoli mepesi kiasi cha kuigharimu timu hiyo. Alisajiliwa na Yanga akitokea African Lyon iliyokuwa Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja.

Kama haitoshi kipa huyo akarudia kazi yake hiyo katika mazoezi ya jana asubuhi ambapo alifuta mabao mengine ya winga mkongwe Mrisho Ngassa na kiungo Thabani Kamusoko.

Hata hivyo karibu na mwisho wa mazoezi hayo Kindoki alipata wababe baada ya kufungwa mabao mawili na mshambuliaji Matheo Anthony na kiungo Maka Edward na kumuacha akijilaumu.

Mshambuliaji Amissi Tambwe alipambana kumfunga kipa huyo lakini aliambulia kugongana naye na kumpa maumivu kipa huyo na kumfanya asimamishe mazoezi na kutibiwa.

Kwasasa Kindoki atakuwa na vita kubwa na kipa mzawa Benno Kakolanya katika kuwania nafasi ya yupi atakuwa kipa namba moja katika kikosi chao baada ya kuondoka kwa Rostand.