Kinara usajili Dortmund atua Arsenal

Muktasari:

  • Sven Mislintat, aliyewaibua wachezaji nyota Ousmane Dembele, Pierre-Emerick Aubameyang na Shinji Kagawa ameacha kazi Dortmund na anatarajiwa kutua Arsenal.

Arsenal imelamba dume baada ya kumnasa kinara wa usajili kutoka klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani.

Sven Mislintat, aliyewaibua wachezaji nyota Ousmane Dembele, Pierre-Emerick Aubameyang na Shinji Kagawa ameacha kazi Dortmund na anatarajiwa kutua Arsenal.

Mislintat  ndiye aliyefanya mazungumzo kwa niaba ya Dortmund kumsajili Emerick Aubameyang.

Pia Arsenal inatarajia kumnasa Mtendaji wa Dortmund Michael Zorc ambaye atakuwa Mkurugenzi wa Ufundi kujaza nafasi ya     Steve Rowley.

Arsenal imewangoa vigogo hao waliodumu Dortmund muda mrefu ikiwa na matumaini ya kupata wachezaji bora kupitia kwao katika usajili.

Mislintat  anatua kwa ‘Washika Bunduki’ baada ya kudumu Dortmund kwa miaka 10 akiwa mkuu wa kitengo cha kuibua vipaji vya wachezaji mahiri.

Dortmund ilitoa taarifa kwamba Mislintat ataondoka katika klabu hiyo licha ya kufanya juhidi za kumbakiza.

“Tulipenda kuwa naye. Amefanya kazi kubwa ya kuibua vipaji katika muda wote wa miaka 10 akiwa hapa. Amesaidia klabu kupata mafanikio akifanya kazi yake kitaalamu,” alisema msemaji wa Dortmund.

Pia alisema vigogo hao walikuwa na uhusiano mzuri kwasababu walifanya kazi kwa umakini, lakini klabu hiyo imeamua kumruhusu kuondoka.

Klabu ya Arsenal imesema aliyekuwa mkurugenzi wake wa ufundi Rowley ameacha kazi baada ya kudumu kwa miaka 25.