Kinachovuruga mambo Simba, Yanga unakijua?

Muktasari:

Kocha wa Azam B, Abdul Mingange, ambaye ni Meja Mstafu, alisema inashangaza kuona viongozi wa klabu hizo wanazungumzia viwango vya wachezaji pamoja na afya zao

MWINGILIANO wa madaraka katika klabu kongwe za Simba na Yanga, umetajwa kuwa ni chanzo cha makocha na wachezaji kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu, hiyo imesemwa na wadau wa soka nchini.

Kocha wa Azam B, Abdul Mingange, ambaye ni Meja Mstafu, alisema inashangaza kuona viongozi wa klabu hizo wanazungumzia viwango vya wachezaji pamoja na afya zao, jambo ambalo si  sahihi.

“Mfano suala la afya ya Shomari Kapombe, jambo hilo lilipaswa kuzungumzwa na daktari wa timu, ndiye aliyepaswa kulitolea ufafanuzi,” alisema Mingange akionekana kugusia suala la Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zacharia Hansppope, ambaye hivi karibuni alimshutumu Kapombe kwa madai amepona ila anaogopa kucheza.

“Soka la Tanzania, linaendeshwa kijanja janja kiasi hata usajili unafanywa na mashabiki na viongozi, mwisho wanampa mtihani kocha kushindwa kupanga kikosi.”

Kocha wa zamani wa Toto Africans, John Tegete alisema: “Ni janga la taifa, mwingiliano wa madaraka na ujuaji unadhoofisha mno soka letu.”

Naye kocha wa zamani wa Njombe Mji, Hassan Banyai, alisema anayepaswa kuzungumzia kiwango cha mchezaji ni kocha kama daktari anavyopaswa kuzungumzia afya ya mchezaji husika.

“Kwa kiongozi kufanya hivyo ni mpaka awe amepewa ripoti maalumu ya mtaalamu wa anachokizungumzia, kinyume na hivyo si sahihi,” alisema.