Kimenya afichua kinachomkwamisha kusepa Prisons

Muktasari:

  • Msimu uliopita mchezaji huyo alikuwa amekubaliana kila kitu na timu za Simba na Azam, lakini baadaye ikashindikana saini yake kupatikana kutokana na dau dogo ambalo alikuwa amewekewa mezani.

BEKI anayekipiga katika klabu ya Prisons, Salum Kimenya amekuwa akihusishwa mara kwa mara kuondoka ndani ya klabu hiyo lakini mwisho wa siku ameendelea kuwepo klabuni hapo kwa misimu minne mfululizo.
Msimu uliopita mchezaji huyo alikuwa amekubaliana kila kitu na timu za Simba na Azam, lakini baadaye ikashindikana saini yake kupatikana kutokana na dau dogo ambalo alikuwa amewekewa mezani.
Mwanaspoti lilimtafuta mchezaji huyo na kutaka kufahamu kwanini amekuwa akihusishwa na kuhama mara kwa mara na dili zake zinashindikana katika hatua ya mwisho.
“Sijawahi kukataa kuondoka Prisons lakini ubaya ni kwamba makubaliano yanakuwa tofauti, sehemu niliyopo sioni ubaya wa kuondoka haraka ila tatizo ni kwamba sijapata ofa nzuri, lakini pia naangalia sehemu ambayo nitalinda kiwango change,” alisema.
Kimenya aliongeza kwamba kuna muda huwa anahitaji changamoto mpya kutokana na kukaa muda mrefu katika kikosi hicho cha Prisons, lakini kumekuwa na mambo mengi katika upande wa ofa.
“Mimi ni kijana mdogo ambaye nahitaji kucheza muda mwingi sana, mchezaji yoyote thamani yake inapanda baada ya kucheza mara kwa mara, kama napata timu ambayo itanipa kile ninachohitaji na uhakika wa namba bila shaka naweza nikaenda, kikubwa wanitafute tuzungumze mimi naweza nikaenda lakini kama tukishindwana nabaki hapa hapa,” alisema.
Kimenya amekuwa na kiwango kikubwa katika kikosi hicho huku msimu huu baada ya timu hiyo kuwa chini ya kocha Abdallah Mohammed, ameweza kumchezesha kama beki wa kulia lakini pia muda mwingine akimtumia kama mshambuliaji.