Kili Stars, Zanzibar Heroes hapatoshi

Thursday December 7 2017

 

By CHARLES ABEL

KIKOSI cha soka cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars,  leo Alhamisi kina kibarua kigumu kwenye Kombe la Chalenji kitakapokabiliana na ndugu zao wa Zanzibar, kuamua hatma yao ya kutinga nusu fainali.

Kili Stars inayonolewa na kocha Ammy Ninje, iliianza michuano hiyo kwa sare tasa na Libya katika Kundi A, hali inayoifanya lazima ishinde leo kwenye Uwanja wa wa Kenyatta, mjini Machakos, Kenya.

Zanzibar Heroes ilianza kwa kishindo michuano hiyo kwa kuichapa Rwanda mabao 3-1 na kushika nafasi ya pili nyuma ya wenyeji Kenya wanaoongoza kwa pointi nne. Ninje amekiri walianza vibaya na kusema wamesharekebisha makosa ya mchezo wa kwanza.

 Kocha wa Zanzibar, Hemed Morocco, naye amekiri mchezo utakuwa mgumu, lakini kasema watapambana.

Rekodi zinaonyesha Kili Stars hupata wakati mgumu mbele ya Zanzibar.

Tangu mwaka 2000, timu hizo zimeshakutana mara sita ambapo  Zanzibar imeshinda mara tatu dhidi ya mbili za Kili Stars, mechi moja zilitoka sare.

Zanzibar iliifumua Bara mabao 4-2 mwaka 2004 kwenye makundi kabla ya mwaka uliofuata kutoka sare ya 1-1, huku Zanzibar ikienda kushika nafasi ya tatu ya mashindano hayo.

2008  Kili Stars iliitambia Zanzibar kwa kuifunga mabao 2-1 pia katika makundi na kurudia tena mwaka 2009 iliposhinda 1-0. Zanzibar ililipa kisasi zilipokutana mchezo wa Mshindi wa Tatu. Mara ya mwisho zilikutana mwaka 2012 na kutoka 1-1 kabla ya Zenji kuibuka kidedea kwa mikwaju ya penalti 6-5.