Kikosi cha mastaa Simba, Yanga waliotwaa ubingwa

Muktasari:

Ubingwa huo ambao Simba imeutwaa kabla ya michezo mitatu msimu kumalizika ni wa 19 kwa klabu hiyo ambayo mara yake ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa msimu wa 2011/2012.

SIMBA ndio bingwa wapya wa soka la Ligi Kuu Bara. Hiyo wala si habari kubwa tena. Msimbazi walijipanga na wameondoka na taji hilo mapema tu. Kesho Jumamosi watakabidhiwa kombe lao pale Taifa, tena kwa heshima kubwa.

Ubingwa huo ambao Simba imeutwaa kabla ya michezo mitatu msimu kumalizika ni wa 19 kwa klabu hiyo ambayo mara yake ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa msimu wa 2011/2012.

Wakati Simba ikitwaa ubingwa, mshambuliaji wake wa zamani, Ibrahim Ajibu amepishana na taji hilo. Alilikosa alipokuwa akivaa jezi nyekundu na nyeupe (Simba) na analibadili na kuvaa za njano na kijani (Yanga), taji likahamia upande wa pili.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Ajibu, mambo ni tofauti kwa Haruna Niyonzima. Jamaa ana upepo na taji hilo kwa sababu ni kama amehama na ubingwa, msimu uliopita aliuchukua akiwa na Yanga na safari hii kafanya hivyo akiwa na Simba.

Kaa chonjo, tuangalie kikosi ambacho kina nyota waliotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara wakiwa na klabu zote mbili za Simba na Yanga kwa vipindi tofauti kama ilivyo kwa Niyonzina na Kelvin Yondani.

JUMA KASEJA

Kaseja mwenye umri wa miaka 33 sasa, alijiunga na Simba mwaka 2003 akitokea Moro United. Kipa huyo anayefahamika pia kama ‘Tanzania One’, alishinda ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza mwaka 2004.

Baada ya kuchukua mwaka huo, akaja tena kuuchukua 2007, 2010 na 2012, mara zote hizo akiwa na Simba.

Sasa hapa katikati mwaka 2008/09 Kaseja alijiunga na Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja na kuisaidia timu hiyo kubeba taji.

RAMADHANI WASSO

Beki huyo Mrundi alizichezea Simba na Yanga kwa mafanikio mkubwa ndani ya miaka yake minne ambayo alikuwa nchini akicheza soka la kulipwa.

Wasso alianza kutwaa ubingwa na Simba mwaka 2004 kabla ya kutua Yanga ambayo alishinda nayo ubingwa mara mbili mfululizo mwaka ya 2005 na 2006.

AMIR MAFTAH

Maftah aliyezaliwa mkoani Mwanza, alianza kuichezea Yanga kisha akajiunga na Simba. Kabla ya hapo alikuwa Kagera Sugar ambayo ndio timu yake ya kwanza kuichezea Ligi Kuu Bara.

Kipindi ambacho Maftah aliichezea Yanga kuanzia 2006 hadi 2010 alishinda mataji matatu (2006, 2008 na 2009) na alipojiunga na Simba alichukua, 2012.

GEORGE OWINO

Mkenya Owino (37) alikuwa ni stopa wa nguvu. Beki huyo wa kati aliyeanza kucheza Simba kisha Yanga, hakutoka moja kwa moja upande mmoja kwenda mwingine.

Owino alishinda taji lake la kwanza nchini akiwa na Simba kwenye msimu wake wa kwanza, 2007. Baadaye aliondoka nchini lakini alipojiunga na Yanga 2009 akitokea Fortuna Düsseldorf ya Ujerumani akachukua tena ubingwa huo.

KELVIN YONDANI

Beki bora zaidi wa kati nchini kwa sasa Kelvin Yondani (33) kiuchezaji anafananishwa na beki wa zamani wa Manchester United, Nemanja Vidic.

Alijiunga na Simba mwaka 2006 na kutimkia Yanga kimafia 2012 akiwa kambi ya Taifa Stars na kusainishwa usiku.

Yondani ameshinda mataji matatu ya ligi mwaka 2007, 2010 na 2012 akiwa na Simba.

Alipotua Yanga aliacha ukame kwa waajiri wake wa zamani na kushinda mataji manne mwaka 2013, 2015, 2016 na 2017.

Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ndio wachezaji waliotwaa mataji mengi zaidi ya Ligi Kuu kwa nyota wanaocheza sasa.

SAID MWAMBA ‘KIZOTA’

Kizota alijiunga na Yanga mwaka mwaka 1988 akitokea timu ya Shirika la Posta la Tabora, enzi hizo likijulikana kama Posta na Simu. Akiwa na Yanga alishinda taji la ligi mwaka 1991 kipindi hicho ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza.

Nyota huyo aliyekuwa mkali kwa mabao ya vichwa, aliichezea Simba 1995 na kuchukua ubingwa kwa awamu nyingine kabla ya kutimkia Uarabuni.

NURDIN BAKARI

Rasta, Nurdin Bakari, alikuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichochukua ubingwa wa Ligi Ndogo mwaka 2007 kabla ya kuondoka 2008 na kujiunga na Yanga.

Mambo hayakumwendea kombo Nurdin akiwa Yanga kwa sababu alishinda ubingwa wa ligi mwaka 2011 na 2013 kabla ya kupotea kwenye soka la ushindani.

HARUNA NIYONZIMA

Niyonzima (28) ambaye alijiunga na Yanga akitokea kwao Rwanda kwenye klabu ya APR mwaka 2011, aliichezea timu hiyo kwa miaka sita na kushinda mataji manne ya Ligi Kuu.

Niyonzima ambaye anatajwa kama fundi wa kuchezea mpira, alishinda mataji hayo 2013, 2015, 2016 na 2017.

Ndani ya msimu huu wa 2017/18 ambao ni wa kwanza kwake ndani ya Simba ambao tayari ni mbingwa utakuwa ni ubingwa wake wa tano nchini japo huu hajautolea jasho kutokana na kusumbuliwa na majeraha kwa karibu msimu mzima.

ZAMOYONI MOGELLA

Historia ipo wazi. Baada ya Sunday Manara kuna Zamoyoni Mogella. Fundi huyu wa mpira alikuwa anajua soka hadi anakera. Angeweza kufanya kile anachojisikia kwenye mechi yoyote.

Mshambuliaji huyo mwenye historia kubwa nchini, alichukua ubingwa wake wa mwisho kwenye klabu ya Simba mwaka 1990.

Mogella alipotua Yanga alitua na neema kwa kutwaa tena ubingwa mwaka 1991.

Mogella mpaka sasa anatambulika kama miongoni mwa vipaji adimu vya soka kuwahi kutokea nchini.

WILLY MARTIN ‘GARI KUBWA’

Gari Kubwa ndiye mchezaji pekee ambaye mbali na kuchukua vikombe na klabu hizo, alikuwa nahodha kwenye vikosi vyote viwili kwa miaka tofauti.

Mshambuliaji huyo, aliichezea Yanga tangu mwaka 1993 lakini mafanikio yake makubwa yalikuwa kushinda taji la Ligi Kuu mwaka 1996.

Willy ambaye alisifika kwa kandanda safi alipojiunga na Simba wakati huo akitokea Majimaji alichukua ubingwa 2001 na kuamua kutundika daluga.

MOSES ODHIAMBO

Odhiambo alivyotoka kwao Kenya alitua Moro United na baadaye akajiunga na Simba mwaka 2007 ambapo kikosi hicho kilitwaa ubingwa wa ligi ndogo na yeye akiwemo. Baada ya kuichezea Simba kwa mwaka mmoja alijiunga na APR ya Rwanda kisha Yanga ikamrejesha 2009 na akaitumikia kwa miaka miwili na kutwaa taji moja la ligi.