Kiggi anukia Ndanda

Muktasari:

  • Kiggi msimu uliopita aliichezea Singida United lakini baadaye aliomba kuvunja mkabata na timu hiyo ili awe huru kuichezea timu nyingine msimu ujao.

KIUNGO Kiggi Makasi anatajwa kujiunga na kikosi cha Ndanda FC ili kuongeza nguvu katika kikosi hicho kwaajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Kiggi msimu uliopita aliichezea Singida United lakini baadaye aliomba kuvunja mkabata na timu hiyo ili awe huru kuichezea timu nyingine msimu ujao.
Kigogo mmoja ambaye yupo karibu na Uongozi wa Ndanda aliliambia Mwanaspoti kwamba jina la Kiggi lipo katika mipango yao na wanafikilia namna ya kumrejesha kwani mazungumzo yamekuwa ya kuvutana katika pande mbili.
“Walitumwa watu kwa mara ya kwanza kwenda kuzungumza naye lakini ilionekana mambo hayajaenda poa na kitu ambacho hivi sasa kinafanyika wanataka Athuman Kambi azungumze nae ili wawe wamsajili kwa msimu ujao,” alisema.
Mwanaspoti lilipomtafuta Kiggi, alikiri kufuatwa na viongozi wa klabu hiyo lakini bado hawajamalizana kutokana na mazungumzo kutofikia sehemu nzuri.
“Ni kweli walinitafuta lakini waliniambia inabidi tuonane ili tukae chini na kuzungumza, bado sijasaini mkataba nao kama tukiafikiana ninaweza nikacheza kwao kwasababu naangalia maslahi,” alisema.
Kama atasaini mkataba na klabu hiyo atakuwa anarejea kwa mara ya pili kuichezea Ndanda kwani alivyotoka kwenye matibabu nchini India baada ya kuumia akiwa na klabu na Simba, timu yake ya kwanza kuichezea ilikuwa Ndanda na kisha akatimkia Singida United.